● Prof.  AbdulKarim Mruma kuiongoza Timu

●Wapewa Hadidu za Rejea 14 muhimu kujenga uchumi wa nchi kupitia madini

● Tanzania kufanya Utafiti wa eneo la asilimia 50 nchi nzima kufikia 2030

● Sekta za kilimo, Afya, Maji na Viwanda kunufaika na utafiti


*Dodoma*


Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amezindua Timu itakayoandaa Andiko la maudhui ya Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri katika hafla iliyofanyika Juni 12, 2024 jijini Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri  Mavunde amesema  kuandaliwa kwa andiko hilo ni matokeo ya maelekezo aliyoyatoa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt. Samia Suluhu  ya kufanyika kwa  utafiti wa kina ili kuboresha eneo hilo na hatimaye kuwawezesha  watanzania wasichimbe kwa kubahatisha.

Waziri Mavunde ameongeza kwamba, mpaka sasa utafiti wa kina kwa nchi nzima umefanyika kwa asilimia 16  ambapo mpango uliopo  kupitia Vision 2030 ni kufikia asilimia 50  ifikapo mwaka 2030.

‘’ Tanzania imejaliwa kuwa na madini mbalimbali lakini bado hatuna uwezo mkubwa wa kubaini kiwango cha madini hayo. Kupitia vision 2030 tutabaini yote hayo,’’ amesema Waziri Mavunde.

Akizungumzia kuhusu  sekta zitakazo nufaika na  utekelezaji wa Vision 2030, amezitaja kuwa ni pamoja na sekta ya  Kilimo , Afya , Maji na Viwanda na kuongeza kwamba lengo ni kuhakikisha Sekta ya madini inajifunganisha na sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo kuziwezesha kukua.

‘’ Hekta milioni 3.6 zimeathirika na tindikali kufanya shughuli za kilimo kuwa ngumu, tukifanya utafiti wa kina utasaidia eneo kubwa la nchi yetu. Tunaona sekta ya madini ina mchango mkubwa wa kuendeleza sekta nyingine, amesisitiza Waziri Mavunde.

Pia, Waziri Mavunde ametaja baadhi ya manufaa yaliyotokana na matokeo ya utafiti  wa kina uliofanywa kwa asilimia 16 nchi nzima  na kubainisha kuwa ni pamoja na kuiwezesha Sekta ya Madini kuongoza kwa kuchangia fedha za kigeni kutokana na mauzo ya bidhaa za madini nje ya nchi ambapo mchango wake umefikia asilimia 56, kuongezeka kwa mapato ya ndani yanayotokana na sekta ya kufikia asilimia 15.

Katika hatua nyingine, Waziri Madini ameikabidhi Kamati hiyo inayoongozwa na Prof. AbdulKarim Mruma hadidu 14 za rejea zitakazowezesha kuandaliwa kwa andiko hilo na  kuitaka kuhakikisha andiko hilo linawezesha utekelezaji wa vision 2030 kutoka na matokeo makubwa nane ikiwemo kusaidia kuongeza mchango wa Sekta ya madini kwenye pato la taifa, kuwezesha upatikanaji wa fedha za kigeni, kuwezesha maendeleo ya viwanda na sekta nyingine na kuwezesha ushiriki wa watanzania katika sekta ya madini.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameipongeza Wizara ya  Madini kwa kufanya  utafiti wa awali Mkoani Dodoma ulionesha uwepo wa aina mbalimbali za madini na kuiomba Wizara kuendelea na utafiti wa kina ili kujua kiasi  cha mashapo  yaliyopo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini Dkt. Mathayo David Mathayo amesema kuwa Vision 2030 itaongeza wigo mpana kwa watanzania kushiriki katika mnyororo unaounganisha sekta nzima ya madini pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya wizara likiwemo Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa ameipongeza Wizara ya Madini kuja na Vision 2030 akisisitiza kuwa umefika muda  wananchi kunufaika na rasilimali  madini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Madini, amesema kuwa wizara ipo tayari kusimamia maono Vision 2030 ambayo yataleta mabadiliko makubwa ya kisekta kwa miaka sita ijayo kupitia hadidu za rejea kama zilivyoainishwa.


*#VISION 2030: Madini ni Maisha na Utajiri*