MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo, amesema benki hiyo imeshuhudia ongezeko kubwa la mapato ya jumla kwa Sh. Bil. 19.27 sawa na asilimia 11.19 hadi kufikia Sh. Bil. 192.1 ikilinganishwa na mwaka 2022 mapato yalikuwa Sh. Bil. 172.83 sawa na asilimia 1.72.

Aliyasema hayo wakati alipozungunza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, kuhusu Mkutano Mkuu ambapo katika mkutano huo aliwasilisha taarifa ya fedha ya mwaka 2023.

Mihayo, alisema kupitia mipango yake ya kimkakati na ubunifu, benki imedhihirisha mafanikio makubwa ya kifedha na ya kiutendaji.

“Ndani ya mwaka 2023, mali za TCB Benki ziliongezeka kutoka Sh. Trilioni 1.285 mwishoni mwa mwaka 2022 hadi Sh. Trilioni 1.389 mwishoni mwa mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 8.1 sawa na Sh. Bil. 103.9.
“Jumla ya mikopo yote iliongezeka kwa Sh. Bil. 73.1 kutoka Sh. Bil.839 mwishoni mwa mwaka 2022 kufika Sh. Bil. 911.2 mnamo Desemba 31, 2023 ikionesha ongezeko la asilimia 8.72,”alisema Mihayo.

Mihayo, alisema ongezeko la mali kulichangiwa na ongezeko la Amana za wateja ambazo ziliongezeka kwa asilimia 12.01 kutoka Sh. Trilioni moja mwishoni mwa mwaka 2022 hadi kufikia Sh. Trilioni 1.112 mwishoni mwa mwaka 2023.

“Katika mapato, TCB Benki ilishuhudia ongezeko kubwa la mapato ya jumla kwa Sh. Bil. 19.27 sawa na asilimia 11.19 hadi kufikia Sh. Bil. 192.1ikilinganishwa na mwaka 2022 mapato yalikuwa Sh. Bil. 172.83 sawa na asilimia 1.72.

“Mapato ya riba yalichangia asilimia 79.61 ya mapato yote ya benki huku kiasi kilichobaki kikipatikana kutoka katika kamisheni, ada mbalimbali na shughuli nyingine zilizofanywa na benki.

“Kupitia usimamizi wa kimkakati wa uwekezaji wake. Amana za TCB Benki katika benki nyingine zilishuka kwa Sh. Bil. 55.3 sawa na silimia 33.32, huku Amana za Serikali zikiongezeka kwa Sh. Bil. 44.1 sawa na salimia 42.64; fedha taslimu na salio katika benki Kuu ya Tanzania (BoT), iliongezeka kwa Sh. Bil. 47 au asilimia 41.26.

“Sisi kama benki, dhamira yetu ya kudumisha ufanisi na kumridhisha mteja inatupa hamasa na uthubutu wa kujituma,”alisema Mihayo.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi, Martin Kilimba, alisema “Tukijiandaa na mwaka ujao wa fedha, tunakusudia kuendelea kuboresha ufanisi wetu ili kuwezesha ukuaji wa taasisi hii.

“Malengo yetu ni kuendelea kuboresha mizania, kujenga taswira mpya ya taasisi yetu, kupokea teknolojia ya kidigitali, kufanya uhakiki wa hasara na kusimamia rasilimali watu.

“Tunaamini mambo haya yatatupeleka katika kilele cha mafanikio na kutengeneza thamani kwa wanahisa wetu.”