Chama Cha ACT Wazalendo kimesema mapendekezo ya bajeti kuu ya serikali kwa mwaka 2024/25 iliyosomwa Bungeni na Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba hivi karibuni imegusa matatizo ya kupanda kwa gharama za maisha kwa kuwa ni jambo linalowagusa Watanzania kwa sasa.

Hayo yameelezwa Leo Jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara Isihaka Mchinjita wakati chama hicho kilipokutana na wanahabari kwa ajili ya kuchambua mapendekezo ya Bajeti Kuu ya serikali iliyowasilishwa Bungeni hivi karibuni.

“Hivi sasa, changamoto nyingine inayokabiliwa wananchi wengi ni upatikanaji wa huduma bora za afya, kila kona ya nchi hii Watanzania wanalalamikia upatikanaji wa huduma za afya, ukubwa wa gharama, huduma mbovu, ukosefu wa dawa na vifaa tiba na maeneo mengine hakuna kabisa miundombinu ya huduma za afya” Amesema Mchinjita.

Aidha amesema kuwa maeneo megnine ya kutazama kwenye bajeti hiyo ya 2024/25 ni elimu na sekta ya nishati ya mafuta na gesi asilia, kwani ni maeneo nyeti ambayo yatafanya bajeti hiyo ihusu watu moja kwa moja.

Hata hivyo amesema mchanganuo wa matumizi ya mapato ya bajeti ya mwaka 2022/23 unaonyesha kuwa sehemu kubwa ya bajeti ilitumika kulipa mishahara, kugharamia deni la serikali, pamoja na matumizi mengine kuliko kutekeleza miradi ya Maendeleo ambayo ndio huduma muhimu kwa wananchi walio wengi.

Amesema katika uchambuzi huu pamoja na mambo mengine imeonyesha kuwa serikali haijatoa majawabu ya changamoto zinazowakabiliana wananchi Kwa sasa ya ukosefu wa fedha za kigeni unaotokana na sababu kubwa ya kuwepo kwa urari hasi wa mauzo ya bidhaa na huduma nje (exports) na bidhaa na huduma tunazoagiza kutoka nje (imports).

Sambamba na hayo amesema kwenye uchambuzi wao marekebisho ya kodi, tozo, makato ambayo kwa namna moja yameachwa bila kufanyiwa marekebisho au kuanzishwa mapya ambayo yanaleta maumivu kwa wananchi.

” ACT Wazalendo tumeangazia kwenye maeneo tisa uchambuzi wa Bajeti Kuu ambayo yanaonyesha ni dhahiri bajeti ya serikali haiendi kutoa nafuu, hivyo tumeiita ‘Bajeti ya kwenda kulipa madeni na gharama za utawala huku ikiendelea kuacha maumivu kwa walala hoi” Amesisitiza Mchinjita.