Na. Mwandishi Wetu, Kigoma


Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kusogezwa be mbele kwa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura hadi tarehe 20 Julai, 2024 badala ya tarehe 01 Julai, 2024 iliyopangwa hapo awali.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kigoma leo tarehe 22 Julai, 2024, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele amesema kwamba uzinduzi wa zoezi hilo utafanyika siku hiyo ya Jumamosi tarehe 20 Julai, 2024 mkoani Kigoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB).

Mhe. Mwambegele ameeleza kwamba uamuzi huo wa Tume umetokana na kuzingatiwa kwa maoni ya wadau walioyatoa wakati wa mikutano iliyofanyika Jijini Dar es Salaam na Mkoani Kigoma.

“Tume imezingatia maoni na ushauri wa wadau. Hivyo, zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litaanza tarehe 20 hadi 26 Julai, 2024 badala ya tarehe 01 hadi 07 Julai, 2024, mkoani Kigoma na uzinduzi utafanyika siku hiyo ya tarehe 20 Julai, 2024 mkoani Kigoma ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb),” amesema.

Akizungumzia maoni hayo ya wadau, Mhe. Mwambegele amesema Tume imefanya mikutano tisa ya wadau ngazi ya Taifa mkoani Dar es Salaam kati ya tarehe 07 hadi 15 Juni, 2024 na mkutano mmoja wa wadau ngazi ya mkoa kwa mkoa wa Kigoma uliofanyika tarehe 19 Juni 2024.

Amewataja wadau waliokutana na Tume kuwa ni pamoja na Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu, wanawake na Wazee wa Kimila.

“Vyama vya siasa vilitoa maoni na ushauri wa kupatiwa muda wa kutosha kwa ajili ya kuwapata mawakala wa uandikishaji ili mawakala hao waweze kushiriki katika zoezi kikamilifu. Aidha, vyama viliishauri Tume isogeze mbele muda wa kuanza kwa zoezi la uboreshaji ili kutoa fursa kwa wao kuhamasisha wananchi na wafuasi wao kujitokeza katika zoezi hilo,” amesema Jaji Mwambegele.

Amewataja wadau wengine waliotoa maoni kuwa ni pamoja na taasisi na Asasi zilizoomba kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uboreshaji ambazo zilieleza kuwa kibali kinapotolewa na Tume huwa ni muda mfupi kufikia zoezi la uboreshaji kuanza na wakashauri Tume ione namna ya kutoa kibali kwa muda utakaowawezesha kupata fedha kutoka kwa wafadhili ili zoezi likianza nao waanze kutoa elimu hiyo.

Kwa upande wa Taasisi na Asasi zilizoomba kibali cha kuwa waangalizi wa uandikishaji wakati wa uboreshaji, zilieleza kuwa kibali kinapotolewa na Tume huwa ni muda mfupi kufikia zoezi la uboreshaji kuanza na wakashauri Tume ione namna ya kutoa kibali kwa muda utakaowawezesha kupata fedha kutoka kwa wafadhili ili zoezi likianza nao waanze kazi ya kutazama namna zoezi linavyoendeshwa.

Maoni mengine ya wadau yaliyopelekea Tume kufikia uamuzi huo wa kusogeza mbele tarehe ya kuanza na kuzindua uboreshaji wa Daftari ni yale ya kuishauri Tume ijipe muda wa kutosha kutoa elimu ya mpiga kura kwa wadau na wananchi kabla ya kuanza kwa zoezi lenyewe, ili wananchi wengi waweze kuelewa zoezi husika na hivyo kuwawezesha kujitokeza kwa wingi wakati zoezi litakapoanza.