Na Mwandishi wa NCAA.

Rais wa Shirikisho la wafugaji Nyuki Duniani (Apimondia), Dkt. Jeff Petiz, ametembelea eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kutoa pongezi kwa uongozi wa NCAA kwa jitihada za utunzaji wa hifadhi hiyo ya kipekee duniani ambayo imeendelea kuvutia maelfu ya watalii.

Akizungumza kwa furaha na mshangao, Dkt. Petiz amebainisha  kuwa hajawahi kuona sehemu nzuri kama Kreta ya Ngorongoro maishani mwake baada  wa kuona wanyama  wakubwa maarufu kama  _Big Five_ ambao ni faru, tembo, Simba, Chui, Nyati na wengineo ndani ya mda mfupi wakiwa katika eneo moja wakiwa kwenye mazingira yao ya asili.

“Hakika nimepata uzoefu usiosahaulika maishani mwangu, kuona eneo la pekee lililotunzwa na kuwepo wanyama wa kila aina na kushuhudia idadi kubwa ya wageni ni jambo la kupendeza na hakika eneo hilo kila mmoja anapaswa kulitembelea katika uhai wa maisha yake” alisema Dkt. Petiz.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo aliyembatana na mgeni huyo ameipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhifadhi eneo hilo mashuhuri duniani katika nyanja za utalii, uhifadhi na utamaduni pamoja na kupambana na mimea vamizi na kutoa rai kwa taasisi nyingine za uhifadhi kujifunza kutoka kwa Ngorongoro ili kubadilishana uzoefu.

Ziara hiyo imefanyika katika Kreta ya Ngorongoro ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano wa kimataifa wa wadau wa nyuki (Apimondia) utakaofanyika mwaka 2027, ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano huo mkubwa unaotarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 6,000 kutoka mataifa mbalimbali.

Katika ziara hiyo Dkt. Petiz ameambatana na Rais wa Kamisheni hiyo kanda ya Afrika , Bw. David Mukomana.