Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimefanya uchambuzi wa Bajeti Kuu ya serikali kwa mwaka 2024/2025 na kutoa maoni yake ikiwa na lengo la kutoa uelewa kwa wananchi kuhusu vipaumbele na sheria zilizopendekezwa kufanyiwa marekebisho ya kikodi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Wakili Fulgence Masawe ambapo amesema uchambuzi huu utasaidia kuongeza mjadala kwa jamii Ili mapendekezo hayo yachukuliwe na wabunge katika mjadala wa kupitisha Bajeti.

Aidha amesema kuwa katika bajeti hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa imejikita kwenye matumizi ya kawaida kwa asilimia 70 huku asilimia 30 ndio ya miradi ya maendeleo jambo ambalo ni wazi kuwa hakutokuwa na miradi mipya ikizingatia fedha hizo zinategemewa kutoka kwa wafadhili.

“Ni wazi kuwa wananchi wasitegeme maendeleo makubwa au miradi mipya ya maendeleo kwani bajeti hiyo ni ya matumizi ya kawaida ikiwemo kulipana mishahara, posho, madeni na kununua magari ya kifahari” Amesema Wakili Masawe.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa bajeti hiyo vyanzo vya mapato vimeendelea kuwa vile vile huku wanaochangia bajeti kwa njia ya kodi ni wananchi wachache.

“Kuna haja ya serikali kubuni vyanzo vipya vya mapato, mfano mchango wa halmashauri kwenye bajeti yetu ni mdogo sana, halmashauri nazo zimeshindwa kubuni vyanzo vipya mfano kupima ardhi kwa wingi na kumilikisha wananchi ili kupata kodi ya ardhi,” Ameongeza Wakili Masawe.

Aidha Massawe amesema kumekuwa na uhaba wa fedha za kigeni nchini na kwamba kinachosababisha uhaba huo ni uwiano kati ya bidhaa zinazouzwa nje na zinazoingizwa.

“Serikali inatakiwa kuwa na mkakati wa kufufua na kuhamasisha uzalishaji wa mazao ya biashara kama kahawa, pamba, mkonge na korosho,” amesema

Amesema Serikali lazima iwe na mkakati wa kujenga mazingira rafiki na kuhamasisha wawekezaji wakubwa kuja kuwekeza nchini

Kuhusu deni la Taifa, Massawe amesema kukua kwa deni la Taifa hadi kufikia Trilioni 91.7 kunaashiria kwamba ukali wa maisha unaweza kuongezeka na utasababishwa na ulipwaji wa deni hilo.

Amesema ni maoni yao kuwa ni muhimu kwa serikali kupunguza gharama za uendeshaji ikiwemo posho, maisha ya kifahari na magari ya gharama kubwa ambayo yanaweza kuwa na mbadala wake.

Massawe amesema pendekezo la kuweka tozo kwenye gesi inayotumika kuendesha mitambo, magari na bajaji linarudisha nyuma lengo namba 13 la Malengo Endelevu ya Dunia.

“Lengo hilo limeweka malengo madogo ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuweka mipango ya kisera ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi, tunafahamu nishati ya gesi na umeme ni moja ya nishati zenye madhara ya chini kwenye kuzalisha hewa ya ukaa ikilinganishwa na mafuta ya petroli na dizeli,” amesema

Hata hivyo amesema LHRC inapendekeza kupunguza kodi ya ongezeko la thamani kwenye bidhaa zote zenye uhitaji mkubwa kwenye matumizi ya nyumbani kama vile bidhaa za chakula ili kupunguza ukali wa maisha.

Sambamba na hayo LHRC imetaja Sheria zinazopendekezwa kufanyiwa marekebisho ya kikodi kuwa ni pamoja na sheria ya Kodi ya ongezeko la thamani sura 148, sheria ya Kodi ya mapato sura 332, sheria ya ushuru wa bidhaa sura 147, sheria ya ushuru wa barabara na mafuta sura 220.

Nyingine ni Sheria ya Serikali za Mitaa ya utozaji wa Kodi ya Majengo sura 289, Sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma mwaka 2018, sheria ya korosho namba 18 na sheria ya magari (ada ya usajili na uhamishaji) sura 124.