Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limefuta matokeo ya watahiniwa 357 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi uliofanyika Septemba 5-6 mwaka huu na kuzuia matokeo ya watahiniwa 120 waliopata matatizo na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote.

Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji Mkuu wa baraza hilo Dkt. Charles Msonde Jijini Dar es Salaam wakati akitangaza matokeo ya mtihani wakumaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2018 na kuitaja mkoa wa Dar es Salaam kushika nafasi ya kwanza kitaifa ukifuatiwa na Geita, Arusha, ,Kilimanjaro, Kagera na Mwanza.

Aidha matokeo ya ufaulu kwa mwaka 2018 umepanda kwa asilimia 4.96 ukilinganishwa na mwaka jana ambapo masomo ya Kiswahili, Sayansi, Maarifa ya jamii na Hisabati ufaulu ukiwa juu ya wastani huku takwimu zikionyesha somo la Kingereza kuwa chini ya wastani japokuwa unaendelea kuimarika mwaka hadi mwaka.

Watahiniwa waliofanya mtihani walikuwa 943,318 na waliofanya vizuri ni jumla ya watahiniwa 733,103 ambao kati yao ni wasichana 382,830 ambao ni sawa na asilimia 77.12 wavulana ni 350,273 sawa na asilimia 78.38 ukilinganisha na mwaka jana ambapo ufaulu ulikwa 72% hivyo kuwepo ongezeko la asilimia 4.96.