Imebainika kuwa matumizi mazuri ya Mtandao katika kutoa huduma mbalimbali ikiwemo zile za ofisini kunasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya rushwa kutokana na wahusika kutoonana uso kwa uso.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Internet Society Tanzania ( ISOC) Abibu Ntahigiye katika warsha ya kuwajengea uwezo wanahabari katika matumizi ya mitandao ya Jamii ambapo amesema taasisi za serikali na binafsi zikitumia mtandao zitarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na kwa wakati.

Aidha amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya Teknolojia katika Mitandao ya Jamii kunahaja ya kuangalia namna ya kutumia mitandao hiyo kwa manufaa ya kiuchumi na jamii kupata elimu bora ya matumizi ya mtandao ambapo waandishi ndio daraja la kuifikia jamii kwa kupata taarifa mbalimbali toka ndani na nje ya nchi.

Aidha ameongeza kuwa ISOC imenzishwa kwa lengo la kutoa elimu ya Mawasiliano ya Mitandao ya Jamii ikiwa ni pamoja na kuangalia maeneo ambayo hayapati huduma hizo na kuweza kusaidia kupatikana kwa utumiaji wa simu zao mitandao ya Jamii.

Amesema kuwa matumizi ya Mitandao ya jamii baadhi wanaitumia vibaya kwa kutuma vitu visivyo na manufaa kwa jamii na wakati mwingine inaharibu vijana ambao huiga vitu visivyo na manufaa kwa taifa na jamii.

Sambamba na hayo Ntahigiye amesema kuwa matumizi ya Mitandao ya jamii ikifundishwa kuanzia shule za msingi itasaidia kujenga uelewa mpana na maana ya matumizi ya mtandao kwa kipi sahihi na sio sahihi cha kuweka katika kuangalia manufaa wanayopata kwa maendeleo yao na nchi.

Amesema baadhi ya nchi zimeanza kufundisha wanafunzi namna ya kutumia mitandao kwa kusisitiza kupitia mara mbili kile wanachotaka kuweka kwenye mitandao kabla ya kutuma.

Amesema kutokana na matumizi mabaya ya Mitandao ya Jamii inafanya baadhi ya vijana kukosa sifa za kuajirika kutokana na baadhi yao kukutwa tayari Wana matumizi mabaya ya Mitandao kwa kutuma picha ambazo hazina maadili pamoja na kuandika vitu visivyofaa katika jamii inayowazunguka.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama hicho Nazar Nicholas amesema kuwa kutumia ISOC wameweza kujenga mnara kwa kutumia kikundi wilayani Kondoa Mkoani Dodoma ili kuwezesha kutumia mitandao ya jamii kwani Makampuni Mengi ya kibiashara hayawekezi maeneo yenye watu chini ya 5000.

Amesema kuwa malengo ya ISOC ni kutaka kuhakikisha jamii yote inafikiwa na mitandao ya jamii katika kupata habari mbalimbali za manufaa, kielimu na kujiletea maendeleo.

“Hatuwezi kuacha jamii inayotumia mitandao bila manufaa kwa kutuma au kusambaza taarifa za uongo ambazo haziwezi kusaidia maendeleo ya nchi”amesema Nazar.

Nae Mkurugenzi Mtendaji Taasisi inayojishughulisha katika Uhamasishaji Makundi yaliyopembezoni (TIBA) Marcela Lungu amesema kuwa baadhi ya picha chafu za wanawake zilizo katika Mitandao ya Jamii hazitumwi na wanawake wenyewe bali zinatumwa na wanaume.

Amesema kuwa matumizi ya Mitandao ya jamii kunahitajika elimu kwani baadhi ya wanawake kutokana na kushindwa kuitumia kutangaza biashara zao na kufanya biashara hizo kushindwa kueleweka ndani ya jamii inayowazunguka.