Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imetangaza neema ya kuwasajili wajasiriamali wote nchini wanaojihusisha na utoaji huduma za kemikali kwa gharama ya shilingi elfu hamsini badala ya milioni moja.

Uamuzi huo umetangazwa na Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelis Mafumiko wakati akifunga mafunzo ya siku moja ya waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam yaliyoandaliwa na mamlaka ya Maabara hiyo kwa lengo la kuwawezesha wanahabari kutambua majukumu ya mamlaka ya Maabara hiyo ili Wananchi na wadau wote wapate kuelewa taasisi hiyo na kushirikiana nayo katika mambo mbalimbali ya kijamii.

Sanjari na hayo Dkt. Mafumiko ameweka wazi muda wa majibu ya uchunguzi wa kimaabara wa sampuli yeyote kuwa ni ndani ya siku 21 na si vinginevyo.

“Kwa miaka 122 sasa tumekuwa tukitekeleza majukumu yetu ambayo ni kufanya uchunguzi wa kimaabara na kutoa ushahidi katika mahakama mbalimbali hapa nchini kwa lengo kuu la kulinda amani na utulivu na kutoa haki haswa katika sampuli zinazohusisha makosa ya jinai hivyo kitaalamu majibu ambayo Mkemia mwenye sifa amejiridhisha nayo yanachukua siku 21 tu” Amesema Mafumiko.

Aidha amesema kuwa Maabara hiyo inafanya kazi kwa mujibu wa sheria licha ya sheria namba nane ya mwaka 2016 kifungu O huipa mamlaka ya kuingia popote na kuchunguza chochote kwa masilahi ya umma bado si kila raia anaweza kuomba uchunguzi wa sampuli yeyote.

“Kuna utaratibu wa uchukuaji wa sampuli kulingana na aina ya shauri na muombaji hivyo si kila mtu anaweza kuomba uchunguzi ni taasisi zilizowekwa kisheria ambazo ni Jeshi la polisi, mahakama, ustawi wa jamii, Hospitali teuli, wakili wa kujitegemea aliyesajiliwa na taasisi za utafiti” Ameongeza Dkt Mafumiko.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya usimamizi wa kemikali Dkt. Daniel Ndio amesema licha ya juhudu za Maabara hiyo kuwasajili wadau wote wanaojihusisha na bidhaa za kemikali bado udhibiti wa kemikali hatarishi utabaki mikononi mwa raia wote wenye mapenzi mema na nchi yao.

“Ni kweli tunadhibiti kemikali zisilete madhara kwa raia na mazingira yake lakini ni changamoto inayohitaji ushirikiano wa pamoja kwani huwezi kuwazuia walimu wa masomo ya kemia kutumia tindikali kufundishia kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kumzuia mama asitumie kisu nyumbani kwake”Ameongeza Dkt Ndio.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya sayansi ya Jinai Hadija Mwema akitoa wasilisho lake juu ya vina Saba ( DNA) amesema kila mwanadamu ana vinasaba vyake ambavyo havifanani na mtu yeyote isipokuwa mapacha wa yai moja .

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ilianzishwa mwaka 1897 ikiwa na lengo la kufanya utafiti wa magonjwa ya joto ambapo imeboreshwa hadi kufikia hadhi ya kuwa mamlaka.