Ubalozi wa Marekani hapa nchini umesema unaunga mkono juhudi za kumwezesha mtoto wa kike kujikwamua kiuchumi zinazofanywa na taasisi mbalimbali ikiwemo kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali ili waweza kukabiliana na changamoto za maisha wanazokumbana nazo.

Hayo yameelezwa Jijini Dar es Salaam na Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Imni Patterson katika mkutano wa Girls entrepreneurship Summit ambapo ameeleza kuwa mafunzo hayo yatawapamotisha na utashi wa kujitegemea, kuleta mabadiliko na maendeleo kwa jamii.

Kwa upande wake Mwanzilishi wa Taasisi ya Appss Girl Carolyne Ekyarisima amesema kuwa taasisi hiyo inawawezesha wasichana kuanzia miaka 14-24 kuwa na uwezo wa kutumia teknolojia na ujasiriamali kubuni vitu tofauti tofauti ambavyo wanatengeneza kama biashara zao au kampuni.

Aidha ameongeza kuwa mafunzo hayo yanawasaidia kujipatia shughuli za kufanya ambazo huwaingizia kipato na pia kuwawezesha kuchagua kozi nzuri kwenye masuala ya tehama kutokana na kuwepo kwa idadi ndogo ya wasichana wenye ujuzi kwenye masuala ya sayansi na teknolojia.

Hata hivyo amesema mkutano huo umekutanisha mabinti zaidi ya 70 na hufanyika kila mwaka na unahusisha mabinti tofauti tofauti ikiwemo wale wa Shule za Sekondari ambao wamepitia mafunzo hayo ambayo huwawezesha kutengeneza tovuti na vifaa mbalimbali ambapo huongezewa ujuzi wa kibiashara na kupanua miradi yao.

Kwa upande wake mwanafunzi kutoka shule ya Kibasila Zahara Juma Muhammed ambae amejishindia dola elfu moja toka Ubalozi wa Marekani ameshukuru taasisi hizo pamoja na mashirika ya kimataifa kutoa mafunzo hayo kwani yanaendelea kuwa msaada mkubwa kwa mabinti ambao wanapitia changamoto mbalimbali ikiwemo kuacha masomo na waajiriwa wa kazi za ndani kuweza kujipatia kipato.