Na Anneth Kagenda.

WAKAZI wa Jiji la Dar es Salaam waliohodhi maeneo bila kutoa taarifa na kuamua kuyafanyia shughuli zao binafsi wametakiwa kuacha mara moja tabia hizo badala yake wametakiwa kurishirikisha Jiji ili  maeneo hayo yaweze kuwa ni sehemu ya kuwanufaisha wananchi na si kwa mtu mmoja mmoja.

Wito huo umetolewa Jijini Dar es Salaam na Naibu Meya wa Jiji hilo Abdallah Mtinika wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

Amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu katika Jiji hili ambao wamekuwa wakihodhi maji za Jiji ambazo wanaamua kujimilikisha wenyewe bila kuwepo na makubaliano kati yao na Ofisi husika.

Mtinika alisema, watu wanaofanya hivyo wanaenda kinyume na taratibu pamoja na sheria ya kumiliki maeneo hayo kutokana na kwamba maeneo mengine yanatakiwa kufanya shughuli za kijamii ikiwemo kujengwa shule, masoko, vyoo vya kulipia pamoja na shughuli zingine za msingi kwenye jamii.

“Sasa katika hili, naomba nitoe wito kwamba kwa yeyote mwenye suala kama hili au sehemu ambazo watu wameodhi maeneo Jiji lishirikishwe na wajue kwamba nasi tutawapa ushirikiano”. alisema Mtinika na kuongeza;

“Lengo letu siyo baya ila tunataka  kubaini na badaye tuweze kuyatolea ufafanuzi kwamba eneo hili mtu anaweza kuendelea nalo kwa maslahi binafsi au lipo kwa ajili ya shughuli za kijamii zaidi”. alisema.

Kuhusu hali ya uchumi Naibu Meya alisema, ni kweli hali imedolola na kusema kwamba siyo tu kwa Afrika bali Duniani kote na kwamba hilo halipingiki.

Mbali na hilo pia aliwataka wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kufuata maagizo ya viongozi yanayowataka kutoka ndani na kwenda kufanya kazi kuliko kuendelea kujifungia majumbani.

“Wananchi watoke wakafanye kazi kama Serikali na Rais wetu John Pombe Magufuli anavyoelekeza huku wananchi hao wakiwa makini na kufuata maelekeza ya kujikinga na corona kama Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inavyoelekeza ili tuweze kujikinga.

Hata hivyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanashona balakoa zenye lea mbili ambazo ni salama zaidi kwa ajili ya kujiepusha na maambukizi ya virusi hivyo hatari.