Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi ISAC KAMWELE amesema serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya bandari, ya Dar es salaam ili iweze kupokea meli zote kubwa duniani toka Ulaya, Asia na kuweza kuhudumia nchi zote za kusini mwaafrika na kati.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kukagua miradi hiyo inayosimamiwa na serikali kwa ajili kupanua na kuimarisha miundominu ya bandari ikiwemo magati saba na kuongeza kina cha bahari ili kusaidia kupokea meli kubwa za mizigo na kupakuliwa kwa mafuta kwa muda mfupi.

Waziri Kamwele amesema uboreshaji huo bandari utawezesha meli kubwa kuingia moja kwa moja pasipo kupitia bandari nyingine za nchi jirani ili kuwapunguzia wafanyabiashara gharama walizokuwa wanatumia hapo awali.

“Hapa hapo awali kabla ya ukarabati meli zilikuwa zinashusha mizigo bandari ya Mombasa, na kupakuliwaa mizigo kisha kuwekwa kwenye meli ndogo kwa utaratibu mdogo transhipment na kusababisha gharama kuwa kubwa “amesema Waziri Kamwele .

Hata hivyo Waziri ameongeza kuwa magata manne ujenzi wake umekamilika ila magata matatu yanatarajiwa kukamilika 2021 ambapo
kutakuwa na mafanikio ya biashara ya kusafirisha malighafi zinazolimwa nchini ikiwemo matunda na mbogamboga kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya bandari (TPA) Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema upanuzi wa magata saba manne kati yake yameshakamilika ukijumlisha na gata la magari ambalo linaukubwa wa hekta 7.5 ambalo litakuwa na uwezo wa kupokea magari elfu tatu na kwa mwaka magari laki mbili.

“Tunajipanga kuongeza jitihada ya kuboresha mazingira ya bandari ili kuliteka soko la Ukanda wa Afika Mashariki, COMESA na SADEC ambapo nchi zake zinahitaji kuchukulia mizigo yake kupitia bandari ya Dar es Salaam”amesema Kakoko.

Aidha amesema Mamlaka ya bandari imeingia mkataba na Dangote anatafuta meli ya kusafirisha saruji kutoka mtwara na kuleta Dar es salaam badala ya kupita barabarani itapitia bandarini na atabeba tani milioni mbili kwa mwaka.

Katika hatua nyingine Waziri Isac Kamwele amezindua mifumo ya Tehama ya ERP na e -office ya Mamlaka ya Usimamizi wa bandari (TPA) utakaosaidia kuokoa mapato yasipotee na kutunza nyaraka mbalimbali ikiwemo za wafanyakazi na utendaji wao wa kazi.

Naye Mwenyekiti wa bodi ya (TPA) Prof Ignas Rubaratuka amesema Mifumo hiyo itasadia kufanyika kazi kwa wakati, ulinzi na usalama wa mali, kufanya kampeni za kimasoko uhusiano wa wadau na kujua kuongezeka na kupungua kwa kipato.