Dar es Salaam, 19 Mei 2024 saa 12:00 Jioni:

Kufuatia taarifa iliyotolewa tarehe 17 Mei 2024 na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu kuwepo kwa kimbunga “IALY” katika Bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar, Mamlaka inapenda kutoa mrejeo kuhusiana na mwendendo wa kimbunga hicho.

Mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga hicho kimeendelea kuimarika na bado kimeendelea kusalia katika Bahari ya Hindi kama ilivyotabiriwa awali, hadi ilipofika saa 3 asubuhi ya leo kilikuwa umbali wa takriban kilomita 680 mashariki mwa pwani ya nchi yetu.

Kutokana na umbali huo kutoka nchini, vipindi vya upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa
na mawimbi makubwa yanayozidi mita 2 vinaweza kujitokeza katika Bahari ya Hindi hususan kati ya leo tarehe 19 Mei 2024 na Jumanne tarehe 21 Mei 2024. Vilevile, vipindi vya mvua
vinaweza kujitokeza katika maeneo ya ukanda wa pwani hususan kati ya tarehe 21 na tarehe 22 Mei 2024.

USHAURI: Watumiaji wa bahari na wananchi wa maeneo ya ukanda wa pwani wanashauriwa kuchukua tahadhari na kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.