●Katibu Mkuu aieleza Kamati Mipango kabambe kuiendeleza STAMICO , STAMIGOLD

*Dodoma*

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kupitia kampuni tanzu ya STAMIGOLD leo Juni 11, 2024 limewasilisha mpango wa uwekezaji wa kampuni ya STAMIGOLD kuhusu uendelezaji wa miradi ya madini kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, jijini Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo,Deusdedith Magala amesema kuwa tangu kuanza uzalishaji hadi kufikia Machi, 2024 mgodi umezalisha na kuuza jumla ya wakia 122,964.53 za madini ya dhahabu na wakia 16,662.54 ya madini ya fedha.

Magala ameeleza kuwa mgodi umeendelea na uhakiki na utafiti kupitia njia mbalimbali za ukusanyaji wa taarifa na ukadiriaji  upya wa akiba ya mashapo ya mgodi ambapo mpaka April, 2024 mgodi ulikuwa na akiba ya mashapo ya wakia za dhahabu 114,190 ambazo zitachimbwa kwa miaka mitano.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Nishati na Madini, Mathayo David Mathayo ameitaka wizara  kuisimamia na kufuatilia kwa karibu  kampuni  ya STAMIGOLD  ili iwe kampuni yenye manufaa.

Akizungumza kuhusu  wajibu wa mgodi kwa jamii (CSR),Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa amesema kuwa wizara imepokea maoni yaliyowasilishwa na kamati kuhusu mapitio ya kanuni za CSR na kuzifanyia kazi ya kuziboresha itakapobidi.

Naye , Katibu Mkuu Wizara ya Madini,Kheri Mahimbali amesema Malengo ya Wizara ni kuipeleka mbali  Stamigold ili uwe mgodi mkubwa utakao tambaa sehemu mbalimbali ndani ya nchi pamoja na kutambulika na taasisi kubwa za fedha.

STAMICO ilianzishwa rasmi mwaka 1972 kwa lengo la kuwekeza kimkakati katika miradi ya madini na uvunaji wa  rasilimali madini ndani ya  mnyororo mzima wa sekta ya madini.