Kilimanjaro.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewapongeza viongozi wa Wizara ya Maji kwa kusimamia na kufanikisha vema utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Same -Mwanga – Korogwe.

Makamu wa Rais ametoa pongezi hizo alipokagua Mradi huo na kushuhudia wananchi wakianza kunufaika na maji yanayotokana na Mradi wa Maji wa Same – Mwanga – Korogwe ambao umefikia asilimia 95. Aidha ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kufanikisha ujenzi wa Kituo cha kupoozea Umeme cha kuhudumia mradi huo.

Aidha Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha vijiji vyote vinavyozunguka mradi huo vinanufaika na maji safi na salama yatokanayo na mradi ili waweze kutunza vyanzo vya maji na miundombinu ya mradi huo.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Same na Mwanga kuanza kutumia vema maji hayo kwa kuhifadhi mazingira ikiwemo kupanda miti katika maeneo yao. Aidha amewataka viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuandaa malambo kwaajili ya kunywesha mifugo ili kulinda mradi huo wa maji dhidi ya unyweshaji mifugo katika chanzo cha mradi huo.

Makamu wa Rais amewahimiza wananchi wanaozunguka mradi wa Same – Mwanga – Korogwe kuhakikisha wanakuwa walinzi wa mradi huo ili uweze kudumu na kuwanufaisha kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso amewataka watendaji wa sekta ya Maji kuhakikisha wanawaunganisha wananchi wa Mwanga na Same huduma ya maji kwa wakati. Pia amewasihi watendaji katika sekta hiyo kuzingatia utoaji wa ankara sahihi kwa wananchi wakati Wizara ikiendelea na utaratibu wa kufanikisha mita za maji za malipo ya kabla.