Aendelea kusisitiza juu ya uongozi wake wa falsafa ya 4R.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewakumbusha viongozi na watanzania wote ya kuwa chimbuko la kuunda kamati ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki jinai ni kutoka Ilani ya ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025.

Chama Cha Mapinduzi kupitia ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025 ilituagiza serikali kuhakikisha tunalinda na kuimarisha misingi ya utu, usawa, haki na uongozi bora ” Alisema Rais Samia.

Rais Samia ameyasema hayo mara baada ya kupokea Taarifa ya Kamati ya Kuunda Mkakati wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Mhe. Balozi Ombeni Sefue.

Akiendelea kuzungumza kupitia hotuba yake iliyosheheni maono chanya, Rais Samia amesema serikali ya awamu ya sita anaiongoza kwa falsafa ya 4R ambayo inaelekeza kwa pamoja kujikita kwenye maridhiano, kuimarisha kustahimiliana, kuleta mageuzi na kuendelea kujenga upya Taifa letu la Tanzania.

Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa katika kuimarisha utendaji na mifumo ya haki jinai nchi nzima, aliunda tume mwezi januari mwaka 2023 ambayo mnamo mwezi julai, 2023 ilikuja na mapendekezo 363 yaliyoelekeza kwenye utekelezaji wa kutenda haki, kuimarisha vyombo vya haki jinai na kutekeleza falsafa ya 4R.