Na Anneth Kagenda

TIMU ya Mpira wa Miguu ya Mzimuni imefanikiwa kuibuka kidedea kwa kujinyakulia kombe, pesa taslimu sh. 150,000 pamoja na jezi ambapo timu hiyo iliingia fainali dhidi ya timu ya Mwananyamala mashindano yaliyoandaliwa na Jumuia ya Wazazi Wilaya ya Kinondoni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Fainali hizo zilichezwa Jijini Dar es Salaam katika Viwanja vya Barafu vilivyopo Manispaa ya Kinondoni Kata ya Magomeni ambapo mshindi wa pili Mwananyamala alipata zawadi ya sh. 100,000 (laki moja).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi waliokuwepo katika mtanange huo walisema kuwa tangu awali timu shiriki zilionekana kufanya vizuri lakini mwisho wa siku Mzimuni na Mwananyamala wakaibuka kuingia fainali.

Mwenyekiti wa Wazazi Wilaya ya Kinondoni Profile Massawe  alitoa pongezi kwa timu zote shiriki na kusema kuwa ni wajibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Jumuia ya wazazi katika Wilaya yake ya Kinondoni.

“Nipende kusema kuwa mbali na hilo pia ni wajibu wetu kuifanya jamii iwe salama, watoto wetu na wengine kuwa salama na hii itasaidia vizazi vyetu kujua kuwa Nchi bila vijana hawa haiwezekani kuwa salama na haiwezi kuwa endelevu,” alisema Mwenyekiti UK. Na kuongeza;

“Lakini pia tunampongeza Diwani wa Kata hii Noordin Butembo ambaye kwa namna moja ama nyingine amekuwa mstari wa mbele pia kuhakikisha jambo hili linafikia muhafaka kama hivi mlivyojionea wenyewe,”.

Alisema kuwa kilichomalizika kwa maana ya  fainali hizo ni mwendelezo wa jitihada za mwaka 2023 zilizoanzishwa na Jumuia ya Wazazi na wao wakaipokea na kuanza kuikimbiza lengo likiwa ni Chama (CCM) kuendelea kuinua vipaji huku lengo lingine ni kulifanya Taifa kuwa mstari wa mbele.

Diwani Butembo alisema kuwa mashindano hayo yalifanyika vizuri na vijana waliyatendea haki na kusema kuwa ni wakatimuhafaka kwa kila mtu kutimiza wajibu wake  kama mtanzania.

“Mbali na hilo nipende kuishukuru Jumuia ya Wazazi kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Wilaya kwa kuiteua Kata yangu kwani tunav viwanja takribani sita hivyo wangeweza kuchagua kiwanja kingine ila wakaona inafaa hapa, lakini pia mimi ni mzazi na ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Jimbo la Kinondoni hivyo inapotokea michezo kama hii lazima niwepo,”.

Naye Katibu wa Jumuia hiyo Jonson Kashasha, alitoa pongezi nyingi kwa viongozi wote walioshiriki kufanikisha mashindano hayo hadi kufikia tamati na kupatikana mshindi na kusema kuwa hiyo ni katika kuendeleza jukumu waliopewa viongozi hao na Chama na kusema kwa Rais Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi kuendeleza vipaji hivyo wanamuunga mkono

“Lakini hatutaishia hapa badala yake Juni 23, mwaka huu tutakuwa na bonanza lingine Jimbo la Kawe na hapa nipende kusema kuwa tumejipanga vizuri kuhakikisha nalo linafana zaidi na hii ni katika mwendelezo wa kuinua vipaji kwa vijana wetu,” alisema.