Dodoma.

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeelezea Mipango yake ikiwemo kuendelea kuwawezesha Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini, huku msisitizo ukiwekwa kwenye ununuzi wa mitambo na huduma za uchorongaji ili kuwasaidia kupata taarifa za miamba, hatimaye wachimbe kwa tija.

Hayo yalielezwa  Juni 24, 2024 na Meneja Uwezeshaji Uchimbaji Mdogo kutoka STAMICO Bw. Tuna Bandoma kwenye Wiki ya Madini inayokwenda sambamba na Kongamano la Wachimba Madini, Mkutano wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA) pamoja na  maonesho ya madini na vifaa vya uchimbaji inayoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Center jijini Dodoma.

Aliongeza kwamba, mitambo hiyo itawahudumia zaidi wachimbaji wadogo wenye leseni hai huku akitaja huduma hiyo kutumia gharama ndogo ambazo itamhitaji mchimbaji kuchangia, ambazo ni nafuu ikilinganishwa na uhalisia wa gharama za uchorongaji.

Akizungumzia mgawanyo wa mitambo hiyo, Bandoma alisema ugawaji wake umezingatia maeneo yenye idadi kubwa ya shughuli za uchimbaji mdogo ikiwemo Mkoa wa Geita na uwepo wa miradi ya mashirika makubwa ili kusaidia  kuhifadhi mitambo hiyo.

Vilevile, akizungumzia kuhusu uwezeshaji wa kifedha, Bandoma alisema STAMICO itaendelea kuimarisha taarifa za wachimbaji wadogo ili waweze kuaminika na kukopesheka na taasisi za fedha.

Naye, Muhasibu kutoka FEMATA Bw. Gregory Kibusi alitumia fursa hiyo kuipongeza STAMICO kwa kuendelea kuwa karibu na wachimbaji wadogo katika kuwawezesha kujiinua kiuchumi kupitia mitambo ya uchorongaji.

STAMICO imeendelea kutekeleza  majukumu  yake ya kuwasimamia  na kuwaendeleza  wachimbaji wadogo  kwa kutoa elimu ya uchimbaji bora unaotumia teknolojia ya kisasa, kuandaa mikutano  inayowakutanisha na wadau wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuleta mitambo  ya uchorongaji maalum  kwao inayowasaidia kujua kiwango cha rasilimali  katika maeneo yao ya uchimbaji.