MAKAMU mkuu wa Chuo kikuu huria nchini (OUT) Profesa Elifas Bisanda, ameliomba jeshi la polisi nchini kuwafikisha mahakamani haraka iwezekenavyo watuhumiwa 17 waliokamatwa wakijaribu kuwafanyia mtihani wanafunzi mbalimbali chuoni hapo.

Profesa Bisanda,ameyasema hayo mapema leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari akizungumzia kukamatwa kwa watuhumiwa hao .

Profesa Bisanda amesema wao kama chuo wapo tayari kuwapa ushirikiano jeshi la polisi ikiwemo vielelezo.

“Sitaridhika kuambiwa kuwa Polisi wanaendelea na upelelezi,kwani maofisa wa Usalama wa Taifa walishudia matukio haya Dhahiri hivyo hayahitaji Upelelezi Zaidi,nawakakishia taarifa hii pia tutaipeleka Polisi Makao makuu,ofisi ya IGP,na Ofisi ya Rais kwa ufatiliaji”Amesema Profesa Bisanda.

Kuhusu hatua kwa waliowatuma ,Profesa Bisanda,amesema Chuo hicho kinasheria na kanuni za mitihani ambazo zitatumika kushughulikia wale waliowatuma hao mamluki kuwaandikia mitihani na Mamlaka za chuo zitawahoji wahusika na wakikutwa na hatia,basi wataadhibiwa kulingana na kanuni.

Akizungumzia jinsi walivyokamatwa watuhumiwa hao, amesema kutokana na udhibiti mzuri wa usalama wa mitihani chuoni hapo,ikiwemo kuwepo kwa maofisa usalama wa Taifa kwenye vyumba vya kufanyia mtihani walifanikiwa kuwakamata wakiwa wamefoji vitambulisho kwa a watahiniwa kwa lengo la kutaka kuwafanyia mtihani.

“Utaratibu wa kuingia kwenye chumba cha mtihani uko wazi ambapo kila mwanafunzi utakiwa kuwa na kitambulisho cha picha yake,au kutumia kutumia kitambulisho cha chuo au pia cha Taifa”amesema

Hata hivyo,Profesa Bisanda,amesema katika kukabiliana na vitendo hivyo,chuo kinajiandaa kuwasajili wanafunzi wote kwa alama za Vidole,ili kuhakiki kila mtahiniwa kwa mashine maalumu ya utambuzi wa alama za vidole katika vituo vyote vya mitihani.


“Hatuwezi kukubali mtu yeyote ahitimu kwa kufanyiwa mitihani na watu wengine,na hili tunatoa tahadhari,mamluki yeyote asijaribu kuonyesha sura yake kwenye vyumba vyetu vya mtihani”