Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Thobias Makoba wakati akifungua kongamano la Uhuru wa kujieleza na sheria ya Vyombo vya Habari
Mratibu wa THRDC Taifa Wakili Onesmo Olengurumwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye Kongamano la Uhuru wa kujieleza na Sheria ya Vyombo vya Habari.

Serikali imesema ipo kwa ajili ya kushirikiana na waandishi sio kushindana hivyo itaendelea kuboresha mazingira ya kisera na kisheria ili kuimarisha zaidi Sekta ya Habari nchini.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na  ambapo amesema Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi kuhusu Uhuru wa kujieleza.

Akifungua Kongamano hilo lililoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria wa Marekani (ABA) Makoba amesema chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumeshuhudiwa mabadiliko makubwa katika tasnia ya Habari kiasi cha kutoa Uhuru mkubwa wa Vyombo vya Habari na kujieleza.

“Awamu  ya Sita ya Rais Dkt. Samia  tumeona mageuzi makubwa kwenye Sekta ya Habari nchini. Serikali tunaamini kwenye mashirikiani na sio Mashindano. Kama Serikali tupo tayari kupokea maoni ya kuboresha kwa maslahi  ya tasnia hii,” Amesema Makoba.

Kwa upande wake Mratibu wa THRDC Taifa Wakili Onesmo Olengurumwa amesema lengo la kongamano hilo ni kujadili Sheria zinazosimamia vyombo vya habari na Uhuru wa kujieleza na kubainisha changamoto na jinsi ya kuzitatua.

Amesema Mtandao wa THRDC wameshafanya uchambuzi wa kesi 30 na kubaini kuwa Sheria ya Makosa ya Mtandao inaongoza kwa kuvunja Haki ya kujieleza kwani imepeleka watu wengi mahakamani kwa tuhuma za makosa ya uchochezi na kusababisha taharuki.

Ameongeza kuwa wanataka kifungu cha 16 cha Sheria hiyo kifanyiwe mabadiliko kwani kimewapeleka watu wengi mahakamani na gerezani, kwamba ni lazima wajadili na Serikali kuona mabadiliko yanafanyika.

“Sheria ya Makosa ya Mtandao imevunja sana Haki ya kujieleza, watu wanakamatwa kamatwa hovyo bila kufuata utaratibu. Hivyo tumetoa mapendekezo yetu ya namba ya kuboresha Sheria zetu. Tunahitaji kuundwa kwa tuma ya pamoja ili kuzifanyia marekebisho ziendane na Wakati,” amesisitiza Wakili Olengurumwa.

Hata hivyo amesema kuwa wanapoelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani, Sheria ya Uchaguzi inatakiwa kufanyiwa mabadiliko kwani inaminya Uhuru wa Vyombo vya Habari katika kuripoti taarifa za Uchaguzi.

“Tunapoelekea kwenye Uchaguzi ni Wakati wa kuwa na Uhuru wa kweli na wazi, kwani bila hivyo wananchi watashindwa kutoa maoni yao,” ameeleza Wakili Olengurumwa.

Hata hivyo amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kufikisha vilio vya wananchi kwa Serikali yao, hivyo ni lazima vilindwe kuliko kuundiwa Sheria za kuvikandamiza.