Na Anneth Kagenda

SERIKALI imesema kuwa imejipanga vizuri katika kuhakikisha inafanya maboresho mazuri na ya kudumu katika Barabara zake kwa kuzifanyia matengenezo pamoja na kuziwekea lami katika Mkoa wa Mpwani hivyo kuwataka wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha barabara hizo zinajengwa kwa viwango vilivyowekwa kwa manufaa ya wananchi.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Miundombinu) kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Rogatus Mativila, mara baada ya kutembelea katika maeneo mbalimbali ambako barabara zinatengeneza akianzia Utete.

“Hapa Utete ambapo naona ujenzi unaendelea vizuri na tumesisitiza barabara ijengwe  kwa ubora na kumalizika kwa wakati kwa manufaa ya wananchi lakini pia ipo ya kilometa 32 ambayo inachanganywa udongo na kemiko na hii inakaa muda mrefu,” alisema Naibu Injinia Mativila na kuongeza;

“Lakini hatukuishia hapo katika kuhakikisha Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inatimiza mahitaji yake kwa wananchi, tumekuja hapa Muhoro, kutembelea daraja linalounganisha kwa kilomita 32 na hili usawa wake utakuwa mkubwa kwenda juu ili maji maji au mafuriko yasivuke kwenda maeneo mengine kwani tunatarajia kuwekwe tuta moja kwenda juu,”.

Alisema kuwa tayari mkandarasi amepewa maelekezo kuwa wanataka daraja lenye ubora ambalo hata baada ya kumalizika litakaa muda mredu sana bila kuleta tatizo lolote.

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini- Tanzania (TARURA) Injinia Leopold
Runji Pwani, alishukuru kwa ujio wa kiongozi huyo na kusema kuwa anaamini lengo kuu la Serikali katika kutatua kero za wananchi linatimia kwani serikali imekuwa ikiweka nguvu kubwa kwa katika kuhakikisha inatatua kero za wananchi wake katika kuwaletea maendeleo.

Alisema kuwa daraja la Muhoro ambalo awali lilijaa maji ya kutisha hivi sasa limepata ufumbuzi wa kina kwani wanaamini baada ya matengenezo hayo kuisha basi wananchi wataendelea kuishi kwa amani huku wakiendelea kutumia barabara zao bila matatizo na kwa muda mrefu.

“Tunaipongeza sana Serikali yetu kupitia Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani anafanya kazi mzuri, anaweka jitihada kubwa katika kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo makubwa katika nyanja tofauti tofauti kwa ajili ya maendeleo wa Watanzania wote,” alisema Injinia Runji, na kuongeza;

“Lakini pia ni shukrani zetu za pekee kwa Naibu katibu mkuu  kututembelea na kuona jitiada tunazoendelea nazo na pia tunamwakikishia kwamba maelekezo yote aliyotupatia tutayafanyia kazi bila kupepesa macho na kuhakikisha kila kitu kinaenda kilivyopangwa kwa wakati na kwa ubora kwa manufaa ya wananchi,”.

Baadhi ya wananchi walioshuhudia ugeni na matembezi ya viongozi hao katika maeneo mbalimbali kwa ukaguzi wa kutekeleza miundombinu hiyo walipongeza na kusema kuwa sasa wanaamini kinachofanyika hakina masihala badala yake serikali imejipanga kuwakwamua wananchi kwenye hali ngumu wanayokuwa wakikabiliana nayo ikiwemo mafuriko.