Na Anneth Kagenda.

MKUU mpya wa Wilaya ya Ubungo Hassan Bomboko, amewafunda Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa Wilaya hiyo na kuwambia kuwa anachotarajia kutoka kwao ni kuhakikisha wanamsaidia Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuibuka na ushindi mkubwa kwenye uchaguzi ujao.

Pia amesema kuwa kwa sababu Rais Samia amekuwa akitoa kipaumbele kikubwa kwa vijana Nchini na hasa wale wanaotokana na UVCCM basi Wilaya yake kwa kushirikiana na vijana hao itakuwa mstari wa mbele kuchanga fedha za Rais kwenda kuchukua fomu ya kugombea urais na kwamba fomu hiyo italindwa na vijana wa UVCCM Ubungo.

DC Bomboko ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na UVCCM Wilaya ya Ubungo kwenye Kikao cha Baraza la Vijana kilichofanyika katika Kata ya Manzese.

Amesema kutokana na Rais kuona umuhimu mkubwa wa kuwashika mkono vijana basi na wao hawana budi kuhakikisha wanarudisha fadhira kwa kuhakikisha anashinda kwa kishindo huku Wabunge, Madiwani na wenyeviti nao wakibaki kwenye nafasi zao.

“Haya nimeisha fika kijana mwenzenu, nipende kutanguliza shukrani kubwa na za dhati kwa Mhe. Rais Samia kwa kuendelea kuniamini na kuniteua tena kuwa DC Ubungo hivyo basi hapa hakuna kulala ila ni kazi tu na kwa upande wangu ninadeni kubwa la kuhakikisha kunakuwa na maendeleo makubwa kwa kushirikiana na nyinyi na ninawaahidi kufanya makubwa,”amesema DC Bomboko.

Aidha, amewataka vijana hao kutambua kuwa wao kama viongozi wananafasi kubwa ndani ya chama hicho na kusema kuwa waachane na bifu zisizokuwa na maana badala yake ofisi yake iko wazi kwa yeyote atakayehisi anajambo la kujadili ili kuweza kufanya mambo ya maendeleo.

“Lakini pia niwaambie kwamba nimekuja ubungo nimekuta wabunge, madiwani pamoja na wenyeviti wote ni CCM hivyo kwenye uchaguzi ujao sitakubari kuona makosa yanafanyika badala yake nitahakikisha hali inabaki vile vile kama nilivyoikuta na upande wa mwenge lazima nako nifanye kweli,”.

Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Ubungo Shedrack Makangula, amesema “Jumuia ya Umoja wa Vijana Ubungo tumejipanga vizuri sana na hasa linapokuja suala hili lililoko mbele yetu la uchaguzi kwani tunaamini tutashinda mapema kwa Kata zote, wabunge, Madiwani mpaka Rais”amesema.

Amesema kuwa changamoto imekuwa ikitokea tu kwenye suala zima la kiuchumi kwa vijana ambalo kiukweli halijakaa vizuri na kwamba wanaendelea kujipanga, kuwa imara na kuboresha mawazo yao kiakiri na kifikra.

“UVCCM inapenda kumuomba DC wetu kutushika mkono kwa udi na uvumba, iwe mvua liwe jua, lakini pia hata pale tutakapo kosea tunaomba utukosoe ili tuweze kusonga mbele na kazi iendelee,” alisema Mwenyekiti Makangula.

Katibu wa Siasa na Uenezi Wilaya ya Ubungo Juma Kingshashu, amesema wanampongeza Rais kwa kumteua DC Bomboko kwani wanaamini atafanya mageuzi makubwa katika Wilaya hiyo kutokana na kwamba anaijua vizuri na hao ni vijana wenzake.

Katibu wa Mbunge Noor, alisema kuwa Mbunge huyo alimtuma awambie vijana kuwa na umakini wa hali ya juu wakati wakitekeleza majukumu yao ya kisiasa na kusema kuwa tayari sh. Milioni 15 tayari zimeelekezwa kwa vijana hao lengo likiwa ni katika utekelezaji wa miradi.