Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group katika kuadhimisha siku ya Shinikizo la juu la Damu imeweka kambi ya siku mbili kutoa huduma  ya vipimo, dawa na matibabu bure kwa wananchi wenye maradhi ya moyo Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI tawi la Dar Group Dkt. Baraka Ndelwa amesema huduma hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya  siku ya Shinikizo la Juu la Damu Duniani ambayo kilele chake ni Machi 17, 2024.

Aidha Dkt. Ndelwa amesema katika siku hizo mbili matarajio Yao ni kutoa huduma kwa wagonjwa zaidi ya 500 na kusema kuwa maradhi ya ugonjwa wa Moyo yamekuwa yakiongezeka kila wakati kutokana na jamii kutofanya mazoezi na kuishi maisha ambayo si rafiki kwa afya ikiwemo unywaji wa pombe kupita kiasi na uvutaji wa sigara.

“Tuko hapa katika Hospitali ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete tawi la Dar Group, Dar es Salaam kwa siku mbili lengo likiwa ni kutoa huduma ya vipimo kwa wagonjwa wenye maradhi ya moyo au kwa watejwa wapya ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Shinikizo la Damu Duniani ambayo kilele chake ni kesho Machi 17,” amesema Dkt. Ndelwa.

Ameongeza kuwa huduma wanayotoa inaambatana na utoaji wa dawa kwa wagonjwa bila gharama yoyote sambamba na utoaji wa elimu ya lishe ili kuendana na mfumo sahihi wa chakula kwa ajili ya kuepuka kuyakaribia maradhi hayo.

Dkt. Ndelwa ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili yakupatiwa huduma hiyo kwani wamejipanga vizuri kuwapa huduma bora na ya uhakika.

Kwa upande wake Meneja wa Hetero LAB Ivan Edmund akizungumza kwa niaba ya taasisi ambazo zimeunga mkono huduma hiyo kwa kutoa dawa bure kwa wagonjwa amewaomba wananchi kuhakikisha wanatumia dawa hizo vizuri kwani zikitumika vibaya ni sumu.

“Pia napenda nitoe wito kwa wananchi ambao wanatumia dawa, watumie kwa sahihi kwa melekezo ya daktari na hata wanapomaliza dozi wanatakiwa warudi tena kurudi kwa daktari ili kupata maelekezo mengine na si kufanya tofauti jambo linaloweza kuhatarishia maisha yake.

“Kwa maana dawa hutibu na sumu ikiwa tu itatumiwa tofauti bila kufuata maelekezo ya daktari,” amesema.

Naye mwananchi aliyefika katika kambi hiyo kupata kupata vipimo na matibabu, Paulina Luhedeka (63) Mkazi wa Tataba jijini Dar es Salaam ameshukuru kupata huduma hiyo amegundulika kuwa na tatizo la presha na ameahidi kufuata aliyoelekezwa na daktari ili kukabiliana na changamoto hiyo.