Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe Albert Chalamila amesema namna pekee ya kupata maendeleo kwa Taifa lolote ni kulipa kodi bila shuruti ambapo Serikali ya Tanzania Kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA), itaendeleza oparesheni za kuwabaini baadhi ya wafanyabiashara wa vinywaji wanaoingiza vinywaji nchini visivyothibitishwa na TBS, na wanaofanya biashara hiyo bila  muhuri wa TRA, kwakuwa lengo lao ni kuhujumu uchumi wa nchi.

RC Chalamila ametoa kauli hiyo Leo Mei 22, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu Ujenzi wa uchumi wa Taifa katika mkoa huo, Kwa kuzingatia misingi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongoza nchi Kwa kuijenga upya, kusisitiza Ustahamilivu na maridhiano’ tangu alipoingia madarakani.

Aidha, RC Chalamila amewasisitiza wafanyabiashara, wakuu wa Taasisi na mashirika mbalimbali kupelekea marejesho ya Payee na SDL kwa mujibu wa sheria inayowataka kufanya hivyo Kila tarehe 7 ya kila mwezi, na Kila Tarehe 20 ya Kila mwezi kwa upande wa marejesho ya VAT, ikiwa ni mwishoni mwa mwaka wa fedha 2023- 24.

“Taifa letu linajengwa kwa kodi za Watanzania, tunahitaji Mtanzania yoyote aweze kulipa kodi ili taifa liweze kumudu kupelekea huduma Kwa watanzania, natoa rai hii mbele yenu waandishi wa habari, kuwasisitiza wafanyabiashara na watu wote wanapaswa kulipa Kodi Kwa Sheria ili taifa liweze kusimamia Msingi huo.

“Sanjari na hili kumekuwa na malalamiko makubwa kutoka kwa TRA, kutokana na wafanyabiashara kutotoa risiti za EFD, na hata wanaoamua kutoa zingine zinakinzana na bei halisi ya mtena aliyonunulia bidhaa, nawaasa wafanyabiashara ni muhimu kutoa risiti kwasababu wewe ni Wakala tu wakukusanya Fedha kutoka Kwa mwananchi,” amesema RC Chalamila.