Na Mwandishi Wetu

Mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya ameamuru kukamatwa kwa Mkurugenzi wa kampuni ya TUDELEY, Jensen Natal pamoja na Mwanasheria wa Kampuni hiyo Edward Mrosso kwa kosa la kukwepa kodi ya zaidi ya Milion 700.

Ole Sabaya, ametoa maagizo hayo jana Agosti 16 wakati alipofanya ziara ya kutembelea mashamba ya kampuni hiyo huku akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama Wilayani Hai

Akizungumza katika eneo la tukio, Ole Sabaya alisema kwamba ana taarifa za uhakika kwamba kampuni hiyo imekuwa ikikwepa kulipa kodi ya serikali kwa muda wa miaka saba hadi sasa.

Akitoa maagizo hayo Ole Sabaya aliliamuru jeshi la polisi Wilayani humo kumkamata Natal na Mroso na kuwekwa mahabusu kwa saa 48 na wahakikishe fedha hizo ambazo ni kodi ya serikali zinalipwa huku akiitaka idara ya uhamiaji Wilayani humo kumnyang’anya hati ya kusafiria meneja wa kampuni hiyo bwana Trevor Gifford hadi fedha zitakapolipwa.

“Wewe utaenda ndani ili uje uniambie kuna utaratibu gani wa kodi ya serikali kulipwa na ijumaa asubuhi uwepo ofisini kwangu uniambie kodi ya serikali italipwaje Chukua passport yake ya zamani na sasa nataka pésa hiyo ilipwe ndani ya siku saba na TRA niletewe maelezo hayo.”amesema Sabaya

Kampuni ya Tudeley inamiliki na kuendesha mashamba ya ushirika ya chama cha msingi cha Murososangi yenye ukubwa wa ekari 2,054.