Taasisi inayowalea watoto yatima ya Tanzania kwanza Foundation (TAKWAFO) iliyopo Manispaa ya Temeke Jijini Dar es Salaam wameiomba Serikali ya Dkt. John Magufuli na jamii kwa ujumla kushirikiana kwa karibu katika kuwahudumia watu wenye uhitaji kwa kuwapatia huduma wezeshi ikiwemo elimu, chakula na mavazi kama njia ya kuwakomboa na kimaisha.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa TAKWAFO Bi. Hidaya Shomvi kwenye kongamano la pili lenye lengo la kuwatia faraja Watoto hao lililodhaminiwa na Kampuni ya Cocacola ambapo maadhimisho yalifanyika katika viwanja vya Temeke Mwembe Yanga yaliyoongozwa na kauli mbiu YATIMA WA MWENZIO NI YATIMA WAKO TUWALEE NA TUWAPENDE YATIMA.

Amesema taasisi yao imejikita katika kuwalea na kuwahudumia Watoto yatima na watu wenye mahitaji maalumu pamoja na utoaji wa elimu ya mazingira, afya,ustawi na ujasiriamali kwa watu wa rika zote.

Hata hivyo amebainisha kuwa Kituo chao kimesajiliwa kisheria mwaka 2016 ambapo wamekuwa wakitoa huduma kwa makundi mbalimbali yenye uhitaji kwa sasa wanahudumia idadi ya watoto yatima wapatao 25 ambao huwapatia malezi yaliyo bora ikiwemo elimu.

Hidaya amesema kuwa TAKWAFO imejikita zaidi katika kuihamasisha jamii masuala ya uzazi salama, hatari za matumizi ya madawa ya kulevya, madhara ya mimba za utotoni pamoja na mazingira ikiwemo upandaji wa miti na utunzaji wa mitaro ya maji taka.

Kwa upande wake mtoa mada ambaye ni mtafiti wa masuala ya ujasiriamali Jacksons Stephen ameeleza kuwa uzalendo ni suala mtambuka panapo uzalendo pana uthubutu wa kuona fursa vyanzo vya fursa ni watu kuweza kujitambua.

Aidha amesema kumekuwa na dhana hasi iliyojengeka vichwani mwa watu kuwa ili mtu aweze kuendelea lazima iwe na madigrii mengi jambo ambalo si kweli kikubwa kinachohitajika ni watu kupenda kujitoa kwa kuangalia fursa zinazowazunguka.

Nae Mkurugenzi Msaidizi wa (TAKWAFO) Dora Mushi amesema malengo makubwa ya maadhimisho ni kuwapa faraja watoto wenye uhitaji hususani kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kula nao pamoja kucheza nao na kuwapatia misaada mbalimbali ya kibinadamu.