Dar es Salaam.

 Upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili ofisa wa Programu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti (26) na mtaalamu wa Tehama, Theodory Giyani(36) wameuomba upande wa mashtaka kuhakikisha wanakamilisha upelelezi wa kesi hiyo kwa wakati ili haki iweze kutendeka.

Magoti na Giyani wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la utakatishaji fedha kiasi cha Sh17 milioni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Wakili wa washtakiwa hao, Fulgence Massawe na Anna Henga wameieleza mahakama hiyo leo Jumanne Januari 7, 2020 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Massawe ameeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Janeth Mtega baada ya wakili wa Serikali Mwandamizi Renatus Mkude akisaidiana na Wankyo Simon kuieleza mahakama hiyo upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

“Kama nilivyosema siku ya kwanza washtakiwa hao walipofikisha mahakamani hapa, Desemba 24, 2019 niliomba upelelezi wa shauri hili uharakishwe ili haki iweze kutendeka,” amedai Massawe

“Jamhuri ilitakiwa ipeleleze kwanza, ndio washtakiwa wakamatwe,” ameongeza

Naye Wakili Henga ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa LHRC ameomba upande wa mashtaka kuhakikishe unakamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi hiyo iweze kusikilizwa.

Akijibu hoja hizo, Wakili Mkude amedai upelelezi wa shauri hilo umefikia hatua nzuri.

“Upelelezi wa kesi hii upo katika hatua  nzuri, licha ya jeshi la polisi kuendelea naupelelezi lakini bado kuna vyombo vingine vinahusika katika upelelezi wa shauri hili na hata ukiangalia asili ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa hawa yanahusisha vyombo vingine, hivyo tutahakikisha kuwa upelelezi unakamilika kwa haraka,” amedai Mkude

“Ni rai yetu tutazingatia maelezo haya ili upelelezi wa kesi hii uweze kukamilika kwa wakati na ili hatua nyingine za kisheria ziweze kuendelea.”

Awali, Mkude ameiambia  mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na kwamba wamefikia hatua nzuri ikiwa ni pamoja kukamilisha baadhi ya maeneo kadhaa ya upelelezi.

Hakimu Mtega baada ya kusikiliza Maelezo ya pande zote, ameahirisha kesi hiyo hadiJanuari 21, 2020 itakapotajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa Kisutu, Desemba 24, 2019 wakikabiliwa na mashtaka matatu katika kesi ya uhujumu uchumi Namba 137/2019.

Katika kesi ya msingi, Magoti na Giyani wanadaiwa kushiriki genge la uhalifu.

Kosa wanaodaiwa kulitenda katika tarehe tofauti kati ya Februari mosi na Desemba 17, 2019 jijini Dar es Salaam na  katika maeneo mbalimbali ya ndani ya nchi, ambapo Magoti, Giyani na wenzao ambao hawajafikishwa mahakamani, kwa makusudi walishiriki makosa ya uhalifu ikiwa ni kumiliki programu za kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kufanya uhalifu.

Katika shtaka la pili, washtakiwa hao na wenzao ambao bado hawajafikishwa mahakamani, wanadaiwa siku na eneo hilo, wanadaiwa kumiliki  programu za Kompyuta kwa lengo la kutenda kosa la uhalifu.

Katika shtaka la tatu, ambalo ni kutakatisha fedha, Wakili wa Serikali Mkuu, Renatus Mkude, alidai kuwa Magoti na Giyani, wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Februari mosi na Desemba 17, 2019 katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ndani ya nchi.

Wanashtakiwa hao wanadaiwa katika tarehe hizo, walijipatia Sh17.35 milioni wakati wakijua fedha hizo ni zao tangulizi la kushiriki genge la uhalifu.

Chanzo ni Mwananchi online