Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa vifaa vya Teknolojia ya Habari Mawasiliano (Tehama) na kompyuta 20 kwa shule za Sekondari Mzumbe pamoja na Kilakala zilizopo Mkoa wa Morogoro.

Vifaa hivyo wamefunga pamoja na mashine ya kuchapia karatasi , Internet pamoja na Kompyuta 10 kwa kila shule hizo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi Kompyuta na Vifaa vya Tehama katika shule hizo Mwakilishi wa Katibu wa Tawala Mkoa wa Morogoro Afisa Elimu wa Mkoa wa Morogoro Tullo Fundi amesema kuwa vifaa vilivyotolewa lazima vitunzwe na kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi kujua Tehama.


Amesema kuwa TCRA imetambua umuhimu wa Tehama na kuamua kutoa Kompyuta ambapo kwa Dunia ya sasa Tehama haiepukiki.


Fundi amesema kuwa shule za sekondari Mzumbe na Kilakala zimepata vifaa hivyo kutokana na kufanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne kitaifa hivyo juhudi zinahitajika kuendelea kufanya vizuri.


Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ,Mkuu wa Kanda ya Mashariki wa Mamlaka hiyo Mhandisi Lawi Odiero amesema amesema Mamlaka imekuwa na utaratibu wa kutoa vifaa vya Tehama kwa shule zinazofanya vizuri kitaifa kwa matokeo ya kidato cha nne ambapo kwa Kanda ya Mashariki shule hizo ziko tano.


Mhandisi Odiero amesema vifaa hivyo wamevitoa ni pamoja na matumizi salama ya mtandao.

“Ninaamini vifaa hivi mtatumia na kusaidia maendeleo ya shule kuendelea kufanya vizuri zaidi ikiwa ni kupata wataalam wa Tehama kutokana na kuwekewa msingi ya huduma hiyo”amesema Odiero .


Nae Mkuu wa shule ya Sekondari ya Wasichana Kilakala mkoani Morogoro Mildreda Selula amesema watatuza vifaa hivyo na kuongeza ufanisi katika somo la Kompyuta na wataendeleza juhudi katika usimamizi na kufanya vizuri.


Makamu Mkuu Shule ya Sekondari Mzumbe Edwin Matenga amesema TCRA imeongeza nguvu kwa kuwapa vifaa vya Tehama na kuandaa wataalam katika sekta hiyo.