Na, Aneth Kagenda.

Wananchi wa Kata ya Ndugumbi Wilaya ya Kinondoni wametakiwa kuwa katika hali ya utulivu wakati wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanesco wakiendelea kufanya marekebisho ya nguzo na nyaya za Umeme.

Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na Diwani wa Kata hiyo Thadey Siriamaka Massawe, mara baada ya kukagua zoezi la marekebisho ya nyaya hizo lililokuwa likifanyika kwenye Kata yake na karibu kabisa na ilipo Ofisi ya Kata hiyo.

Mara baada ya kuona mwenendo mzuri na kasi ya hali ya juu iliyokuwa ikifanywa na wafanyakazi hao, amesema kuwa ni vyema sasa wananchi wakawa na uvumilivu wa mda mchache kwani badaye huduma ya umeme itarudi kwenye hali yake ya kawaida.

“Najua wananchi wa Kata yangu watapata wakati mgumu kwa mchana huu lakini nyakati za jioni huduma itarudi katika hali yake ya kawaida kwani Tanesco wanajitahidi kufanya shughuli zao kwa weledi zaidi,” amesema Massawe na kuongeza;

“Lakini pia nimeona ipo haja ya kupitia na kukagua ili kujihakikishia kwamba wananchi wangu hawaadhiriki na marekebisho yanayoendelea lakini pia nitoe pongezi kwa Tanesco kwamba wanafanya kazi mzuri kwa lengo la kuwasogezea huduma muhimu wananchi,”.

Hata hivyo, amesema kuwa ni vyema kwa wananchi kuendelea kutunza na kulinda miundombinu ya umeme kwa madai kuwa kufanya hivyo kutaifanya miundombinu hiyo kuendelea kudumu kwa muda mrefu na kuwaondolea usumbufu wa kukatika katika kwa umeme.