Utafiti uliofanywa na Kampuni ya Refine Data Tech yenye makao makuu yake nchini Estonia umeeleza kwamba ikitokea Uchaguzi Mkuu ukafanyika kipindi hiki Rais Samia Suluhu Hassan angeshinda kwa asilimian 75.


Akiwasilisha maoni hayo ya Watanzania leo Jijini Dar es Salaa, katika mkutano na waandishi wa Habari Meneja Mahusiano wa Kampuni hiyo Sonja Ohra-aho amesema utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita Watanzania wameonyesha kuuami na kukubaliana na juhudi za Rais Samia kwa kipindi chake cha mwaka mmoja cha kuiongoza Tanzania.


Aidha amesema kuwa katika matokeo ya utafiti huo jumla ya Watanzania 8,960 walishiriki katika kutoa maoni haya ambapo wanawake ni asilimia 56 na wanaume asilimia 44 na usajili wa wapiga kura ni asilimia 87.


Ametaja sababu ya Rais Samia kuchaguliwa kwa asilimia 75 kuwa ni kutokana na kuendeleza miradi ya kimkakati ambapo ameeleza kuwa asilimia 67 ya washiriki wamesema Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi ya kimkakati kwa zaidi ya asilimia 61.


“ Sababu nyingine za Rais Samia kukubaliwa na Watanzania ni mapambano yake dhidi ya rushwa ambapo tunaona asilimia 55 ya washiriki wamesema Serikali imejizatiti kupambana na rushwa kwa zaidi ya asilimia 41″Amesema Sonja Ohra-aho, Na kuongeza kuwa


“Kitu kingine ni kusimamia haki, usawa, amani na utangamano, ambapo tunaona kwamba asilimia 39 ya washiriki wamesema Serikali imeweza kulinda haki na kudumisha amani, usawa na utangamano kwa zaidi ya asilimia 91”


Hata hivyo amesema vita dhidi ya Uviko-19 zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na maoni ya Watanzania kuonyesha kuwa asilimia 70 ya washiriki wamesema Serikali imefanikiwa kupambana na Uviko-19 kwa zaidi ya asilimia 61.


Katika upande wa uongozi wa Rais Samia, amesema maoni ya Watanzania yameonyesha kwamba asilimia 76 wanasema ni mzuri, asilimia 14 mbaya na asilimia 10 wastani.


Sambamba na hayo amesema jambo ambalo Watanzania wanavutiwa katika uongozi wa Rais Samia ni vita dhidi ya Uviko-19 asilimia 25, kujenga uchumi asilimia 11, ushirikiano na vyama vingine asilimia 14, utoaji ajira asilimia 4, kusikiliza wananchi asilimia 10 na kuendeleza miradi ya kimkakati asilimia 36.


Ameongeza kuwa ushirikiano wa mihimili ya Serikali, maoni ya Watanzania yameonyesha kuwa asilimia 88 ya Watanzania wamesema Rais Samia amefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 90.


Katika suala la ujenzi wa uchumi kwa mujibu wa maoni hayo asilimia 60 ya washiriki wamesema Serikali imeweza kujenga uchumi kwa zaidi ya asilimia 61 ambapo katika upande wa ushirikiano wa kimataifa, kutokana na kujenga mahusiano ya kimataifa asilimia 80 ya washiriki wamesema Serikali imeweza kukuza ushirikiano wa kimataifa kwa zaidi ya asilimia 61.