Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watu 12 kwa tuhuma za kuhusika katika matukio mbalimbali ya kihalifu.


Akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es salaam ACP Muliro Jumanne Muliro amesema jeshi hilo limemkamata Iddi Omari Ndakae @Chuma Steel kwa tuhuma za kupora pikipiki katika maeneo ya Kigamboni na maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.


Amesema mtuhumiwa akiwa na wenzake tarehe 16.04.2022 alimkodisha dereva pikipiki Jumanne Mpenja kutoka Mbagala charambe kumpeleka Kigamboni, ambapo walipofika Visikini, Kigamboni alimpiga dereva kwa kitu kizito kichwani hatimaye kufariki na kuiba pikipiki yake.


Katika mahojiana ya kina na mtuhumiwa huyo Jeshi la Polisi lilibaini kuwa mtuhumiwa lishiriki katika tukio lingine la kumpiga kwa kitu kizito kichwani kisha kumuua Mkapa Nuru miaka (20-25) tarehe 27.08.2021 aliyekuwa mkazi wa Mbagala Kiburugwa na kumpora pikipiki namba MC186 CXX aina ya Boxer.


“Baada ya kufanya tukio hilo la mauaji mtuhumiwa aliutupa mwili eneo la Visikini Dege Kigamboni ambapo katika ukaguzi wa eneo hilo kumepatikana mifupa idhaniwayo ya binadamu ambayo ni 1. fuvu la kichwa, 2. mifupa 2 ya nyonga na kaptula ya jeans vyote vinavyodhaniwa kuwa ni vya marehemu aliyekuwa anatafutwa muda mrefu”Amesema ACP Muliro nakuongeza kuwa;


Pia amekamatwa Mfaume Donald Kapela (23) mkazi wa Kibiti sokoni ambaye alishirikiana naye na baada ya mahojiano ya kina Jeshi lilifanikiwa kuipata pikipiki ya marehemu MC186 CXX aina ya Boxer na Pikipiki aina ya TVS ambayo imetolewa namba za usajili.

Katika tukio lingine Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam limemkamata Abulaziz Abdallah@Hunter (19) Mkazi wa Chanika Tungini, akiwa na wenzao 9 wenye umri kati ya miaka 13 – 21 wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kujeruhi watu kwa mapanga, kuvunja nyumba usiku na kuiba katika maeneo mbalimbali ya jiji
Jeshi la Polisi linaendelea na operesheni kali dhidi ya vikundi mbalimbali vya kihalifu katika jijji la Dar es salaam na watakaokamatwa watafikishwa katika vyombo vya sheria.