Kamisaa wa Sensa Spika Mstaafu Anne Makinda amesema zoezi la Sensa ya Watu na Makazi 2022 kwa siku ya kuamkia Agosti 23 limefanikiwa kwa asilimia 17.13

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Saalam Makinda amesema kiwango hicho kimevuka malengo waliojiwekea cha asilimia 15 katika ukusanyaji wa taarifa kwa siku hiyo..

Amesema makarani wamefanya kazi ya ziada kwa kuwafikia wananchi na kuvuka kwa malengo ambapo hiyo kasi ni kufikia asilimia 100.

Amesema zoezi litaendelea kwa muda wa siku saba hivyo ni vyema kwa wananchi kuwa na uvumilivu wa kwamba kila mwananchi ni lazima atahesabiwa kwani Sensa ya mwaka huu imeboreshwa.

“Yapo maneno mengi mtaani yanayosemwa kuhusu sensa na wakati mwengine inachanganywa sensa na uchaguzi ninachotaka kusema ni kwamba hii sensa ni siku saba lakini uchaguzi unafanyika siku moja “, amesema Makinda.

Amesema Rais kuitangaza Agost 23 kuwa Siku ya mapumziko ni kuiheshimisha nchi kwa sababu zoezi la sensa ni la umuhimu sana linafanyika kwa miaka 10 mara moja.

Aidha amewataka waratibu wa Sensa wa Mikoa na Wilaya kuweka namba maalum ambayo itatumika kwa ajili ya kueka ahadi kwa watu ambao hawajahesabiwa kuhesabiwa.

Amesema kupiga simu hizo ni bure hazitakuwa na malipo lengo ni kutaja muda watakaokuwepo nyumbani kwao ili wafuatwe kwa lengo la kukamilisha zoezi.

Makinda amesema vishkwambi vipo vya kutosha hata kama ikitokea vimepotea vipo vya ziada kwa ajili ya kukamilisha zoezi la sensa .

Hata hivyo amewataka viongozi wa serikali za mitaa kuwaongoza makarani wa sensa na kwa kila kiongozi mmoja anatakiwa amuongoze karani mmoja.

” Kwa kila kiongozi atalipwa kulingana na kumuongoza karani wala wasiwe na shaka kwani posho zao zipo”, amesema Makinda.