Hamisa Mobeto; ni mwanamitindo maarufu nchini Tanzania ambaye amefichua kuwa mpenzi wake wa sasa ndiye mwanaume pekee aliyewahi kuwa naye ambaye hajaomba kuzaa naye.


Hamisa anasema kuwa, hajawahi kujadili suala la mtoto na mpenzi wake asiyejulikana katika kipindi ambacho wamekuwa kwenye mahusiano.
Vilevile anasema kuwa, kwa sasa ameridhika na watoto wawili ambao tayari anao.

“Kwa hivi sasa siko pia kwenye utayari wa kuongeza mtoto. Sasa hivi niko na watoto wawili, wa kike na wa kiume,” anasema Hamisa ambaye kwa sasa yupo juu kuliko mastaa wote Bongo na kuongeza;


“Hivi sasa najiangazia mwenyewe zaidi. Huko mbele labda baada ya kufunga pingu za maisha kama Mwenyezi Mungu ameniandikia ndiyo ninaweza kuongeza mtoto mwingine, lakini siyo kwa sasa.”
Kuhusu suala la kumficha mpenzi wake, Hamisa anasema kuwa, kwa kawaida huwa hathamini kuyaanika mahusiano yake hadharani.

Hamisa anasema kuwa, wakati mtu anapoamua kuanika mahusiano yake hadharani, basi yanakoma kuwa ya kibinafsi na kuwa ya umma.


“Mimi naamini kama kitu ni chako na Mungu amepanga, basi kitakufikia na hakitakuwa cha kuibiwa. Siamini kama mwanaume anaweza kuibiwa…siyo kama namficha. Mimi na yeye tuko vizuri katika mapenzi yetu. Tunakula, tunatembea pamoja, yaani tuko vizuri,” anasema Hamisa.

Anasema kuwa, siyo sawa kwake kuendelea kuwatambulisha wapenzi wapya kila wanapokuja katika maisha yake huku akibainisha kuwa tayari yeye ni mama wa watoto wawili wenye baba tofauti.


“Tukifika mbele huko kama Mwenyezi Mungu alimuandikia kuwa mume wangu, basi huwenda watu wataanza kumjua. Lakini hivi sasa kama tukiachana? Na nikipata mwingine tena nimtambulishe itakuwaje,” anasema Mama Wawili.

Anabainisha kwamba, kufichua mahusiano hadharani mara nyingi huwafanya watu waache kujizingatia kazi za mtu na badala yake kuzingatia penzi.

Licha ya kutomtambulisha mpenzi wake wa sasa hadharani, Hamisa ameweka wazi kuwa kwa sasa anaogelea kwenye dimbwi la mahaba anayopata kutoka kwake.
Amemtaja mpenzi huyo wake mpya kama; ‘mwanaume mzuri sana’.