WATANZANI wakiwemo kada mbalimbali wamejitokeza kwenye kuwania tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu zinazotarajiwa kutolewa Aprili 13 mwaka huu.

Kada hizo wakiwemo Waandishi wa habari,wafanyakazi wa Ndani,Polisi pamoja na wauguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa kamati ya tuzo hizo, Profesa Penina Mlama, wakati aakitangaza hatua iliyofikikia kwenye kuelekea kwenye utoaji tuzo hizo.

Aidha,Profesa Mlama amesema tuzo za mwaka huu zimeonyesha uwepo wa mwitikio mkubwa wa tuzo hizo ..

“Ushiriki wa kada nyingine katika tuzo hizi umetupa matumaini kuwa taarifa kuzihusu zimewafikia wengi hata wasio wanataaluma, jambo litakalosaidia kuinua vipaji vipya katika uandishi wa fasihi.”Amesema Profesa Mlama,ambaye ni mwandishi wa siku nyingi wa vitabu,

Hata hivyo,Msomi huyo amesema tuzo hizo zitatolewa Aprili 13, siku aliyozaliwa hayati Julius Nyerere, na kutangaza zawadi na kutaja kuwa mshindi wa kwanza ataondoka na kitita cha Sh10 milioni, na kitabu chake kitachapishwa na kusambazwa shuleni kwa gharama za Serikali.

“Kwa upande wa mshindi wa pili, atapata milioni saba na watatu atapewa milioni tano huku washindi wa nne mpaka wa 10 wakipewa vyeti kwa ajili ya kutambua ushiriki wao”Amesema

Awali akizungumzia Tuzo hizo, Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda, amesema mgeni anayetarajiwa kuja kutoa tuzo hizo ni mshindi wa tuzo za Nobel kwenye uandishi wa Fasihi, Profesa Abdulazak Gurnah.

“Ushiriki wa Gurnah katika tuzo hizo kwetu kama nchi ni heshima kubwa kutokana na kujulikana duniani.

“Mnakumbuka mwaka jana katika tuzo hizi mgeni alikuwa Rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano ambaye ni Rais wa kwanza kuhutubia kwa lugha ya Kiswahili katika  mkutano wa Umoja wa Nchi za Africa (AU),” amesema Profesa Mkenda.

Kwa upande wake Mkurugenzi  Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ambao ndio waratibu wa tuzo hizo, Dk Anneth Komba amesema shindano hilo ni endelevu na akiwataka watu kuendelea kuandika vitabu.

“Ni kwa kutambua umuhimu wa fasihi hata katika mitaala iliyoboreshwa Serikali imeingiza somo la fasihi kwa watoto wetu hivyo vitabu vitahitajika, waandishi kazi ni kwenu kuandika vitabu vingi muwezavyo,”amesema Dk Aneth.