Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Suleiman Serera,alipongeza Baraza la Kiswahili nchini(BAKITA)kuendana na kasi ya teknolojia kwa kuvishirikisha vyombo vya habari na kusaidia taarifa zao kuwafikia watanzania wengi hasa vijana.

Dkt Serera ameyasema hayo leo Jijini Dar es salaam wakati alipotembelea Ofisi za BAKITA zilizoko jijini hapa kwa lengo la kujifunza na kuangea na wafanyakazi wa Baraza hilo.

Amesema hatua ya BAKITA kutumia mitandao ya kijamii pamoja na radio mbalimbali ni jambo nzuri ambalo linasaidia umma wa Watanzania kuzifahamu kazi za Bakita vizuri.

“Nawapongeza sana, ujue mtu akiambiwa kuhusu BAKITA anajua ni watu wakizamani lakini kwa jinsi ninavyoona hapa mnavyovitumia vyombo vya habari kama hivi,ni jambo jema sana”Dkt Serera.

Aidha,Dkt Serera, ameisifu BAKITA hasa watumishi wake kwa kuhakikisha wamejipanga kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya sita kwa kukuza Kiswahili.

“Nimepita hapa nimebaini mnakwenda na kasi ya Rais wetu kwa kuhakikisha wanakuza lugha ya Kiswahili ikiwemo kufungua vituo vya Kiswahili Duniani”Amesema.

Hata hivyo,Dkt Serera,ametumia nafasi hiyo kuwataka wakalimani wote waliosomea wa lugha mbalimbali wajitokeze BAKITA ili iweze kuwajua waweze kupatiwa fursa mbalimbali ambazo zinajitokeza.