Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amesema Mradi wa Maji wa Mshikamano Jimbo la Kibamba unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi August Mwaka huu ambapo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza fedha za UVIKO19 kiasi Cha Shilingi Bilioni 2.5 kutatua kero ya Maji Jimbo la Kibamba.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua Mradi huo,RC Makalla amesema Mradi huo unagharimu Shilingi Bilioni 4.8 ikiwa ni Bilioni 2.5 za UVIKO19 na kiasi kilichobaki ni mapato ya ndani ya DAWASA ukihusisha Ujenzi wa Tank la Lita Milioni 6, Ulazaji wa Mabomba na Kituo Cha kusukuma Maji.

Aidha RC Makalla amemuelekeza Mkandarasi kuongeza bidii ili kuhakikisha Ujenzi unakamilika kabla ya Mwezi August Mwaka huu ambapo mpaka Sasa Mradi upo Asilimia 30.

Pamoja na hayo RC Makalla amewasifu na kuwapongeza DAWASA kwa kazi kubwa na nzuri ya utekelezaji wa miradi mingi ya Maji kwa ufanisi.

Hata hivyo amesema kukamilika kwa mradi huo kutatatua kero ya maji kwa wananchi wa Kibamba na kuondoa dhana ya suala la maji kugeuzwa kama siasa.