Wananchi wanaoishi pembezoni mwa Mto  Ng’ombe Kata ya Makumbusho Wilaya ya Kinondoni wameomba kukamilishwa ujenzi wa mto huo pamoja na kulipwa fidia kwa wananchi waliobakia.

Hayo wameyasema leo katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla alipotembelea mto huo kujionea hali halisi ya mto huo na kusikiliza kero za wananchi wa maeneo hayo.

RC Makalla amesema tayari wameshaongea na mkandarasi anarudi kazini na aendelee na kazi kwani ameshalipwa zaidi ya asilimia 65 na Novemba 22 mradi ukamilike pamoja na kazi aliyoongezewa ya barabara ianze na kurekebisha sehemu ambazo sio nzuri na wanaosimamia wasimamie ipasavyo.

Aidha amemtaka mkandarasi kuanza na Maeneo ambayo ni korofi ambapo wananchi wanaingiliwa na maji ayafanyie kazi kwa haraka kwani Rais anazunguka kupata wafadhili wa kukamilisha miradi ya Maendeleo.

Hata hivyo amewataka walioliolipwa fidia waondoke  katika maeneo ya mto huo ili kupisha mkandarasi aendelee na kazi ya ujenzi na wao kuepuka kukumbwa na madhara hususani kipindi hiki mvua zinaponyesha.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Kinondoni Alberto Kindole akitoa taarifa ya mradi huo wa utekelezaji wa ujenzi wa kingo za mto Ng’ombe amesema mradi huo una urefu wa kilomita 8.5 na mfereji wa kiboko wenye urefu wa km 2.5 umetengewa zaidi ya Bilioni 32 ambapo hadi sasa zimeshalipwa zaidi ya Shilingi bilioni 20 kwa mkandarasi toka china Henan International Cooperation group (CHICO).

Amesema Mradi huo unaurefu wa kilomita 2.5  wa Mto Sinza unapita kwenye jumla ya kata 2 na mitaa 9 ambapo Fidia bilioni 3.2 awamu ya kwanza watu 298 na awamu ya pili na bilioni 3.5 watu 125.

Katika ziara hiyo pia ametembelea mradi wa ujenzi Tenki la maji Kibamba litakalokuwa na ujazo wa lita milioni 6 na  utanufaisha wananchi laki moja na elfu themanini.

Aidha amesema mradi huo unatarajia kukamilika Agosti 17 mwaka huu hivyo wenyeviti wa mitaa wawahamasishe wananchi kuunganishiwa maji.

Hata hivyo amewataka wananchi wa Kibamba Wasingoe mita ili kurahisishiwa huduma maana wakiziondoa watakosa maji na mradi ukikamilika siasa za maji kibamba zitaisha.