Na Anneth Kagenda

Rai kubwa na yenye msisitizo imetolewa kwa wanachama wote wenye sifa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi za Chama na Jumuia na kwamba fomu zitatolewa bure Wilayani hapo bila malipo yoyote.

Kadharika, imeelezwa kuwa kwa mujibu wa ratiba ya Uchaguzi ya uchukuaji na urejeshaji fomu ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa Chama na Jumuiya zake itakuwa ni kuanzia Julai 2-10/2022.

Rai hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam jana na Katibu wa Wilaya ya Kinondoni James Mgego wakati akizungumza na Mwandishi wa habari hizi.

Kabla hajaendelea kuzungumzia ratiba hiyo Katibu Mgego, alitoa taarifa ya awali kuwa bado chama kiko kwenye ratiba ya uchaguzi ambapo Juni 4-11, kulikuwa na utoaji fomu ngazi ya Jumuia na Juni 13-20 kulikuwa ni ngazi ya Kata.

“Zoezi limeenda vizuri kama lilivyopangwa kwa Chama na Jumuiya na sasa tupo kwenye Jumuia na vikao ngazi ya Kata na zoezi la vikao linaendelea vizuri hatuna changamoto kwani kwenye zoezi la vikao pia tunaendelea vizuri,” alisema Katibu Mgego.

” Na kuhusu suala hili lilopo mbeke yetu la kuchukua fomu ni wakati muhafaka kwa wana-CCM wote katika Wilaya ya Kinondoni wanaojua wanasifa kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali,” alisema Katibu Mgego na kuongeza;

“Ifahamike kwamba fomu zinatolewa bure bila malipo na ikumbukwe kwamba Wilaya tumejipanga vizuri katika kuhakikisha zoezi hili linaenda vizuri na linafika tamati yake vizuri kwa hiyo hatuna shaka katika hili,” alisema Katibu.

Amesema kuwa Chama hakiruhusu wale wote wanaokuja kuchukua fomu au kurudisha kuja na wapambe, mgoma, kelele za watu au bodaboda na mambo mengine kama hayo.

“Lakini pia mbali na hayo pia kama nilivyosema wapambe na watu wengine hawaruhusiwi kwenye zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu mgombea anaweza kuchukua fomu na kurejesha siku hiyo hiyo lakini ndani ya mda uliopangwa lakini pia moja ya sifa ya mgombea sharti awe mwanachama wa CCM, ajue kusoma na kuandika na pia awe Raia wa Tanzania,” alisema Katibu huyo.