Shirika la Posta Tanzania na Kampuni ya usafirishaji TUTUME wametia saini ya makubaliano ya biashara ya usafirishaji wa sampuli za kibaiolojia utakaoongeza tija na hatimae mapato ndani ya shirika, serikali lakini pia kumnufaisha mwananchi kwa kupata huduma bora.

Akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa utiaji saini huo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema Ushirikiano huo ni wa manufaa kwa pande zote mbili lakini kikubwa sana ni wa manufaa kwa wananchi;

“Kwa upande wa shirika la posta Tanzania ushirikiano huu utaongeza wigo wa utoaji huduma kwa jamii kutoka kwenye huduma za kiuchumi pekee hadi za kijamii pamoja na viwango vya ubora na utoaji huduma yaani quality of service standards”

Aidha Waziri Nape amesema “Kwa upande wa serikali ushirikiano huu utasaidia kuongeza malengo yake ya kuimarisha huduma za Afya mpaka vijijini kupitia taasisi hizi mbili zinazosaini makubaliano ya ushirikiano leo”

Waziri Nape amesema kwa upande wa TUTUME, ushirikiano huo watapata nafasi ya kushiriki kuihudumia jamii kwa kuwa sehemu ya usafirishaji wa sampuli za damu kutoka katika maeneo ya kukusanyia sampuli hadi kwenye Maeneo ya kupokelea sampuli shirika la posta Tanzania litahakikisha sampuli hizo zinafikishwa zinapotakiwa kufika.

Mbali na hayo Waziri Nape amesema Shirika la posta linafanya kazi ya kuwasaidia wananchi kwa ushirikiano na kampuni ya TUTUME kwenye maeneo ya Afya ili kuongeza kasi na ufanisi pia kuwafikia wananchi wengi zaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu

Hata hivyo Waziri Nape amelitaka shirika la Posta Tanzania kutumia fursa hiyo ya uwekezaji kwenye kilimo katika kusafirisha vitu mbalimbali kama mbegu;

Kwa upande wake PostaMasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo amesema serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata huduma za Afya kwa urahisi hususani huduma za uchunguzi wa Afya zao imelipa jukumu shirika la Posta Tanzania la usafirishaji wa sampuli za maabara kutoka vituo vya Afya kwenda maabara za uchunguzi na kurejesha majibu yake baada ya uchunguzi