Wizara ya Afya katika kutekeleza jukumu na dhamana ya kusimamia utoaji wa huduma za afya zenye ubora hapa nchini imeweka vipaumbele mbalimbali ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na bobezi nchini.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Sarekalini Englibert Kayombo imeeleza kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa  katika sekta ya Afya ngazi zote za utoaji wa huduma za Afya katika Hospitali za Mikoa, na imeimarisha miundombinu ya kutolea huduma, kwa kuhakikisha uwepo wa vifaa tiba na vifaa vya ugunduzi wa magonjwa na uwepo wa madaktari bingwa nchini.

“Mfumo wa utoaji wa huduma za afya unahitaji huduma za kibingwa ziweze kutolewa katika ngazi ya hospitali za Mikoa inafahamika kuwa ili huduma za kibingwa ziweze kutolewa hospitali inatakiwa kuwa na miundombinu wezeshi (infrastructure), watoa huduma bingwa (specialists), uwezo wa kuchunguza na kugundua magonjwa (diagnostics), uwepo wa vifaa tiba wezeshi na uwepo wa bidhaa za afya za kibingwa” Amesema Kayombo.

Na kuongeza kuwa “Huu ni uwekezaji mkubwa uliofanywa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuhakikisha mwananchi anapata huduma za kibingwa katika ngazi ya Mkoa”

Aidha amesema Malengo makuu ya huduma  za Mkoba za Kibingwa ni pamoja na Kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi Kuwajengea uwezo wataalamu wa fani mbali mbali waliopo ngazi za chini za kutolea huduma na Kuibua wagonjwa wanaohitaji huduma za ubingwa bobezi katika hospitali za Kanda, Maalum na Taifa.

Ameongeza kuwa Wizara itatoa huduma za kibingwa za Mkoba katika kambi 6 kwenye Mikoa ya Morogoro, Lindi, Songea, Geita, Tanga na Kigoma ambapo Madaktari bingwa kutoka katika hospitali za rufaa za Mikoa, Kanda, Taifa na Maalum watashiriki kutoa huduma 12 za kibingwa ambazo ni huduma za Ubingwa wa akina mama na uzazi, watoto, Upasuaji, Magonjwa ya ndani, Upasuaji Mifupa, Dharura na ajali, Radiolojia, Utoaji wa dawa za ganzi na usingizi, Afya ya akili, huduma za Utengemao, huduma za Macho na huduma za kinywa na Meno.

Hata hivyo Kambi hiyo itafanyika kuanzia tarehe 29 April mpaka tarehe 11 Mei, 2024 kuanzia saa 2 asubuhi mpaka saa 10 jioni na itafanyika kwa awamu mbili, na kila awamu itadumu kwa muda wa wiki moja. Awamu ya kwanza itafanyika katika Mikoa ya Geita, Songea na Tanga kuanzia tarehe 29 Aprili hadi tarehe 4 Mei, 2024 na awamu ya pili itafanyika katika Mikoa ya Lindi, Morogoro na Kigoma kuanzia tarehe 06-11 Mei, 2024.

Kampeni hii yenye kauli mbiu ya “Madaktari Bingwa wa Rais Dkt. Samia Tumekufikia, Karibu Tukuhudumie” ina lenga katika kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za kibingwa katika maeneo yao.

Sambamba na kambi hiyo ya Madaktari Bingwa wa Rais, Dkt Samia katika Hospitali za Mikoa, Wizara inaendelea na Kampeni ya kuimarisha ubora wa huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto katika ngazi za Halmashauri na baadhi ya vituo vya afya kupitia kampeni ya Madaktari bingwa wa Mama yenye kauli mbiu ya “Jiongeze tuwavushe Salama” iliyozinduliwa mwaka 2023 kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI, Mikoa na Halmashauri.

“ Kampeni hii inafanyika katika hospitali zote za halmashauri, ambapo madaktari bingwa wa huduma za Uzazi, Mama na Mtoto wapo katika Hospitali za Halmashauri kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalam na kutoa huduma za uzazi, mama na watoto” Ameongeza Kayombo.

Na kuongeza kuwa “Kampeni hii katika Hospitali za Halmashauri itaendelea kwa muda wa wiki nane hadi tarehe 28 Juni 2024, katika Mikoa yote 26 na Kanda zote kwa wakati tofauti. Kila hospitali ya halmashauri imepokea timu ya madaktari bingwa watano, ambao watafanyakazi na kutoa mafunzo elekezi kwa muda wa wiki moja kwa kila hospitali.”

Amesema Wizara inatoa wito kwa viongozi wote wa ngazi ya Mikoa na Halmashauri za Wilaya, Wabunge na Madiwani kuwapokea madaktari bingwa wetu na kuhamasisha jamii/wananchi kufika hospitali kupata huduma stahiki.