Dar es Salaam, 04 Mei 2024 saa 05:00 Asubuhi: 


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” kilichopo karibu na maeneo ya pwani ya nchi yetu. Hadi kufikia saa 9 usiku wa kuamkia leo, Kimbunga “HIDAYA” kilikuwa katika eneo la bahari takriban kilomita 125 kutoka pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi), kilomita 93 kutoka pwani ya Mafia na kilomita 128 kutoka pwani ya Dar es salaam kikiwa na mgandamizo wa hewa wa kiasi cha 985 hPa na kasi ya upepo unaofika kilomita 120 kwa saa. 

Tangu usiku wa kuamkia leo, matukio ya upepo mkali na mvua kubwa zinazosababishwa na uwepo wa kimbunga “HIDAYA” yameendelea kujitokeza ambapo hadi kufika saa 3 asubuhi, kituo cha hali ya hewa cha Kilwa Masoko (Lindi) kimeripoti mvua ya jumla ya kiasi cha milimita 111.3 kwa kipindi cha masaa 6 yaliyopita.

Kiwango hiki cha mvua ni kikubwa sana ukizingatia kuwa wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko ni milimita 96.6 tu.  Hivyo kiasi cha mvua kilichonyesha ndani ya masaa 24  katika kituo cha Kilwa Masoko  ni takribani asilimia 115 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko. Viwango vya mvua vilivyopimwa katika vituo vingine katika kipindi hicho ni milimita 90.7 kwa Mtwara na milimita 85.3 katika kituo cha hali ya hewa Naliendele (Mtwara). Kiwango cha mvua cha milimita 90.7 kilichonyesha Mtwara ndani ya masaa 24 ni takriban asilimia 168 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa Mtwara (milimita 54).

Vipindi vya mvua kubwa bado vinaendelea katika maeneo hayo ya ukanda wa pwani ya kusini. Kwa upande mwingine, katika vituo vya hali ya hewa vya Mtwara, Kilwa, Zanzibar, Tanga na Dar es Salaam upepo mkali unaozidi kilomita 50 kwa saa umeweza kupimwa katika nyakati tofauti kuanzia usiku wa kuamkia leo hadi asubuhi hii.

 
Aidha, kimbunga “HIDAYA” kinatarajiwa kuendelea kusogea karibu zaidi na ukanda wa pwani ya nchi yetu huku kikipungua nguvu taratibu kuelekea usiku wa kuamkia Jumapili tarehe 05 Mei 2024.
Kimbunga “HIDAYA” bado kinatarajiwa kuendelea kusababisha matukio ya vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa pwani hususan mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es salaam pamoja na kisiwa cha Unguja na maeneo ya jirani.

Vilevile, matukio ya mawimbi makubwa baharini yanatarajiwa kuendelea kujitokeza katika ukanda wote wa mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi.


USHAURI: Wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari kubwa na pia kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila baada ya masaa matatu, na mara kwa mara kila inapobidi.

Imetolewa na: 
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.