Chama cha ACT Wazalendo kupitia kwa Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Hamidu Bobali katika Uchambuzi wa Bajeti ya wizara kwa mwaka 2024/25 kimesema mfumo wa sasa wa kugharamia Elimu ya juu, Elimu ya Ufundi na ufundi stadi pamoja na vyuo vya matibabu bado inaweka vikwazo kwa watoto kupata elimu kwa kadri ya vipawa, vipaji na uwezo.

Hayo amesema Leo Jijini Dar es Salaam wakati akichambua bajeti ya Wizara hiyo ambapo amesema kupanua wigo wa wanafunzi kuendelea na masomo, kupata ujuzi au ufundi ni lazima Serikali ibebe gharama za ada, malipo ya mafunzo kwa vitendo, Fedha za vitabu na viandikwa ili kuondosha matabaka ya watoto wa masikini na mtajiri kwenye kuwania elimu.

Aidha, amesema ACT Wazalendo ikipewa madaraka itafuta madeni ya mikopo yote ya miaka ya nyuma iliyotolewa kwa Wanafunzi wa Elimu ya juu na itatunga sheria kuhakikisha kuwa mikopo ya Elimu ya juu itakuwa ni kwa ajili ya gharama za kujikimu tu (Meals & accomodations).

Sambamba na hayo ameitaka Serikali itenge Bajeti ya Shilingi bilioni 50. 2 ili kuajiri walimu elfu 65 kila mwaka kwa miaka 5 mfululizo kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la Uhaba wa walimu ambao kwasasa nchi ina upungufu wa Walimu 279,202 kwa shule za Msingi na sekondari.

Ameongeza kuwa kitendo cha Serikali kuchelewesha fedha za ruzuku ya kuendesha shule kinasababisha kudhhofisha uwezo wa shule hizo kutoa Elimu kwa ubora unaotarajiwa. Kwakuwa fedha hizo ndio zinatumika kununua vitabu, kufidia ada, kugharamia mitihani, ukaguzi na uthibiti ubora.

A “kiwango kilichopangwa cha ruzuku ya shilingi 10,000 na 25,000 kwa mwezi kwa mwanafunzi katika shule ya msingi na Sekondari mtawalia. Hakitoshelezi kugharamia mahitaji na kufikia lengo la kutoa elimu bora bali ni bora Elimu hivyo ni vyema Serikali kuongeza bajeti ili kuongeza ruzuku kufikia sh. 25,000 na 58,000 kwa mwanafunzi wa shule za msingi na sekondari” Amesema Bobali.

Aidha ameitaka Serikali kusimamia utekelezaji wa uamuzi wa kumrejesha mtoto wa kike shuleni baada ya kujifungua, kukomesha ukatili dhidi ya watoto ili kuhakikisha watoto wanakuwa huru kushiriki na kupata Elimu na pia ametaka Serikali iweke mkazo kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia ili kupunguza umbali na kutoa vivutio kwa wanafunzi.

Hata hivyo wameitaka Serikali kuhakikisha sekta ya Elimu inasimamiwa na Wizara moja ili kuondoa mgongano katika usimamizi, utekelezaji na uwajibikaji. Kwa sasa Sekta ya Elimu inasimamiwa na Wizara tatu Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kwa sehemu ndogo Wizara ya Maendeleo ya jamiii, Jinsia na Makundi Maalumu.

Amesema katika utekelezaji wa sera ya elimu kumekuwa na muingiliano katika utawala wa elimu, ujenzi wa miundombinu na utoaji wa miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa Elimu.

Bobali ameshauri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iachiwe majukumu yote yanayohusu masuala ya elimu kuanzia ngazi ya awali mpaka chuo kikuu ili kuwajibika ipasavyo kuanzia, utungaji wa sera, utekelezaji na usimamizi.