Dar es Salaam.


Kampeni rasmi za kumnadi  Dkt. Faustine Ndugulile kugombea nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika ambapo ni kwa mara ya kwanza Tanzania inatoa mgombea wa nafasi hiyo zimeanza na kuungwa mkono na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania.

Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa Kampeni hiyo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba amewaomba Mabalozi wa nchi Rafiki na Tanazania kuwashawishi Mawaziri wao wa Afya Kumpigia kura Dkt. Faustine Ndugulile katika kinyang’anyiro hicho ili aweze kushinda.

Aidha amesema tayari wanamtaji wa kura 23 kutoka Nchi 16 za SADC ambazo zimeaihidi kuipigia kura Tanzania pamoja na nchi nyingine saba walizofanya nazo mazungumzo  hivi karibuni na kuonyesha nia ya kuichagua Tanzania katika Nafasi hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Tanzania inafanya vizuri sana katika sekta ya Afya hususani katika kukabiliana na magonjwa yasiyoyakumbukiza,huduma za mama na mtoto,Upasuaji mbalimbali,matibabu ya moyo na mifupa ambapo anaamini kwamba Tanzania itatoa mchango mkubwa kwa Afrika katika kutunga sera bora za Afya zitakazo isaidia Afrika kupiga hatua endapo Mgombea wake atashinda katika kinyang’anyiro hicho.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinafanya vizuri sana duniani katika mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kuimarisha huduma za afya ya uzazi mama na mtoto, Tanzania tumefanikiwa kupunguza vifo vya wanawake wajawazito kwa zaidi ya asilimia 80”. Amesema Waziri Ummy.

Amesema, Tanzania ina mfumo mzuri sana wa kuimarisha huduma za Afya ngazi ya msingi kuanzia Zahanati, Vituo vya Afya pamoja na Hospitali za Halmashauri, hivyo itakwenda kubadilishana uzoefu huo na nchi nyingine za Afrika.

“Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika ambae anamaliza muda wake wa miaka 10 anatokea nchini Botswana ukanda wa SADC, kwa Tanzania ni Mara ya kwanza tunagombea nafasi hiyo na tunaamini kabisa tutashinda nafasi hiyo kutokana na aina ya mgombea ambae tumemuweka.” Amesisitiza Waziri Ummy.

Naye Dkt. Faustine Ndugulile ambae ndio mgombea wa nafasi hiyo amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupendekeza jina lake na kuridhia kugombea katika nafasi hiyo.

“Nafasi hii inasimamia nchi 47 katika Bara la Afrika, Tanzania tunafanya vizuri sana katika Sekta ya Afya na tuna mafanikio makubwa ya kuigwa, tunataka na sisi tuende tukayaeneze yale mazuri yetu kwa wengine ili kuweza kusimama pamoja”. Amesema Dkt. Ndugulile.

Dkt. Ndugulile amebainisha vipaumbele vya nchi ambavyo ni pamoja na kuendelea kuboresha huduma za Afya katika kupunguza vifo vya mama na mtoto ambalo ni eneo Tanzania imefanya vizuri, nchi nyingi za Afrika bado wana changamoto hiyo.

Hata hivyo amesema Tanzania inataka ikasimamie kujenga mifumo imara ambayo itaweza kuhimili athari za magonjwa ya milipuko pamoja na majanga mengine ambapo kwa Bara la Afrika limeathirika sana na magonjwa hayo.